Shaukatali Hussein ni kijana mwenye ari ya kutaka kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri kwa kutengeneza mifano (prototype) ya magari au “bajaji” na pikipiki zinazotumia nishati ya umeme badala ya mafuta.
Hussein ameamua kuwekeza katika teknolojia hii ambayo bado jamii haijatambua umuhimu wake. Hatahivyo, anasema, “mabadiliko hayaepukiki.”
Umoja wa Ulaya (EU) umependekeza kuwa ifikapo mwaka 2035, uuzaji wa magari katika masoko makubwa ujikite katika magari ya nishati ya umeme pekee, badala ya dizeli na petroli.
Nchi kadhaa, ikiwemo Afrika Kusini zimeshatengeneza mifumo na sera ili kuchochea mabadiliko haya. Wavumbuzi kama Hussein, ambao wanatengeneza mifano ya magari hayo nchini Tanzania, wanaona fursa licha yakukumbwa na changamoto lukuki.
“Mabadiliko mapya kuyapokea siyo rahisi sana na mtu pia ukimwambia hizi teknolojia mpya zina faida kidogo au zaidi inakuwa vigumu kuona pia,” anasema Shaukatali, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Robotech Labs inayojishughulisha na teknolojia na uvumbuzi.
Endapo magari au bajaji za umeme zitaanza kutumika nchini, kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza gharama za usafirishaji lakini pia kuleta ushindani wa kibiashara miongoni mwa watengenezaji na wasambazaji wa vyombo hivyo vya usafiri.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa jijini Dar es Salaam nakuchapishwa tarehe 22 April 2021 katika jarida la sayansi Springerlink. Mbali na utafiti huo, Hussein anasema, “Kuna soko na kuna mahitaji maalumu sana, kwa sababu tunapoangalia mazingira sasa hivi na mambo ya kuongezeka kwa joto duniani, hilo ni muhimu pia japokuwa watu hawalielewi sana.”
Stella Mwinuka, Mhandisi na Msimamizi katika maabara ya Robotech, anasema ni umuhimu kuanza kuwapatia watu elimu juu ya tehama katika kuleta suluhu bayana ili kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Hii inaenda sambamba na kutolewa kwa elimu ya kutosha kwa jamii, itakayo wasaidia hususani watumiaji bajaji na pikiki kujiingizia kipato.
Bi Mwinuka anasema, “Hapa kwetu, tunawafundisha vijana ujuzi wa kompyuta na tehama ili kwa kutumia ujuzi huo waweze kutengeneza (solution) masuluhisho kwenye jamii, lengo hasa likiwa ni kuwaandaa na kuawapa ujuzi wa kutengeneza ufumbuzi kwa vitendo kwa ajili ya kutatua matatizo kwenye jamii.”
Hapa Tanzania kuna mitazamo kinzani juu ya sera, ajira na kimasoko kuhusu magari haya. Kwa mijibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Springerlink, inaoenekana pamoja na kwamba madereva teksi ambao ndiyo watumiaji muhimu zaidi, wanaonyesha utayari mkubwa wa kukumbatia magari yenye kutumia teknolojia ya umeme, lakini hata hivyo wanatakamagari yajayo kuwa na sifa zinazofanana za uendeshaji kuliko magari yao ya sasa yanayotumia mafuta.
“Kwa kuwa soko la Tanzania liko makini sana katika swala la bei[…]iwapo miundombinu kama hiyo inatekelezwa, kunahitajika mchanganyiko wa magari yanayofaa, yenye ushindani wa gharama ili kuwezesha mabadiliko ya soko la magari kuelekea usambazaji wa umeme,’’ watafiti wanashauri.
Miezi minne iliyopita, Waziri wa Ufaransa wa Biashara ya Nje na Mvuto wa Kiuchumi Franck Riester alizindua rasmi magari ya umeme nchini Tanzania, ambayo ni rafiki kwa mazingira yaliyoundwa na E-Motion Africa, ila yamejikita katika sekta ya utalii.
“Tanzania imeingia katika uchumi wa kati na mabadiliko kama haya hayaiachi nchi nyuma kwasababu tuko kwenye mnyororo wa kimataifa kiuchumi. Haya mabadiliko iwe changamoto kwa watunga sera katika kutazama fursa zilizopo na pia kudhibiti athari zitokanazo na madiliko haya,’’ anasema Dkt Hildebrand Shayo, mchumi na mhadhiri katika Chuko Kikuu Huria cha Tanzania(OUT)