- Tangazo -
Home Teknolojia Wanasayansi, msipopata fursa magazetini au redioni, tumieni intaneti vizuri: mtaalamu

Wanasayansi, msipopata fursa magazetini au redioni, tumieni intaneti vizuri: mtaalamu

- Tangazo -

Dar es Salaam. Wanasayansi nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto katika kutafsiri tafiti wanazozifanya na kuziwasilisha kwa lugha rahisi kwa jamii, hususani kupitia vyombo vya habari. Hivyo, wameshauriwa kuwekeza katika kushirikiana kwa ukaribu na waandishi wa habari na kuongeza bidii katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano(Tehama) ili kupanua wigo wa mawasiliano kwaajili ya maendeleo.

Katika kufanikisha hilo, watafiti kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameshirikishwa mbinu mbalimbali ili kufikia lengo, walipokutanishwa na waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari nchini.

Mtaalamu katika mawasiliano ya sayansi kutoka SciDev.Net, Dkt Charles Wendo, amewashauri watafiti wa chuo hicho kutumia fursa zitokanazo na ukuaji wa Tehama katika kuwasilisha taarifa zao kwa jamii ili ziweze kutumika katika kufanya maamuzi na kuboresha sera za maendeleo.

Dkt Wendo alizungumza katika warsha iliyofanyika wiki iliyopita katika shule ya Tehama ya UDSM, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu namna ya kurahisisha sayansi na kuiweka katika lugha inayoeleweka kwa jamii na watunga sera.

“Ukilinganisha na miaka iliyopita, hivi sasa kuna mbinu nyingi zinazoweza kutumiwa na wanasayansi katika kuwasilisha ujumbe muhimu kutoka kwenye tafaiti zao ili watunga sera waweze kuzielewa na kuzizingatia,” alisema.

“Kuna mitandao ya kijamii, mfano Facebook, Twitter na WhatsApp ambazo huwafikia watu wengi na kwa haraka. Wakati mwingine huwa ni ngumu kwa watafiti kupata nafasi ya kufikisha taaria kupitia vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni. Katika hali hii, mawasiliano kwa kutumia intaneti ni muhimu,” alishauri Dk Wendo.

Katika warsha hiyo, iliyofadhiliwa na Shirika La Kimataifa la Maendeleo la Sweden(Sida), watafiti walipata wasaa wa kufafanuliwa mbinu mbalimbali kupitia mazungumzo na Daktari wa binadamu aliyejikita katika mawasiliano na habari za kitabibu, yaani medical journalism, Dkt Syriacus Buguzi.

Dkt Buguzi alielezea kwa kina changamoto zinazowakabili watafiti katika kuwasiliana na wahariri/waandishi wa habari ili kuweza kufikisha taarifa zao za kitafiti hasa zile zinazokuwa zimechapishwa katika majarida mbalimbali ya kisayansi.

“Kuna changamoto pande mbili; kwa waandishi wa habari na kwa watafiti wenyewe. Kuna umuhimu kwa watafiti kuwa na mahusiano endelevu ya kitaaluma na waandishi wa habari. Pia, waandishi wa habari wejikite katika kubobea kwenye kuandika habari za sayansi kwa kujiendeleza kimasomo na kiutendaji,’’ alisema Dkt Buguzi, ambaye mara kadhaa ametoa mihadhara kwa waandishi wa habari na wanasayansi kuhusu uandishi wa habari za kitabibu; katika chuo kikuu cha tiba na sayansi shirikishi(Muhas).

Mratibu wa ushirikaano wa UDSM na Sida, Dkt Latifa Mbelwa alisema warsha hiyo imewafumbua macho watafiti katika kuona fursa ya kuweka wazi taarifa zao za kitafiti ambazo mara nyingi hubaki katika majarida ya kisayansi bila kutafsiriwa kwa lugha rahisi.

“Ili watafiti waweze kunufaika zaidi katika hili na kuifikia jamii, inabidi huu ushirikiano kati ya waandishi wa habari na wanasayansi udumishwe,’’ alishauri Dkt Mbelwa.

Mwandishi wa habari kutoka Daily News, Bi Mary Ramadhani, aliwashauri watafiti kujiweka karibu na waandishi wa habari, tofauti na ilivyozoeleka kwamba ni vigumu kuwapata watafiti kuzungumzia tafiti zao kwenye vyombo vya habari pale wanapohitajika.

“Kuna wakati mwingine waandishi wa habari hushindwa kabisa kuandika habari kuhusu tafiti fulani kwasababu watafiti hawataki kuzungumza. Ili kuboresha haya mahusiano kati ya hizi taaluma mbili(uandishi wa habari na sayansi)inabidi kubadili mitazamo yetu na kuwa na fikra chanya juu ya vyombo vya habari,’’ alisema.

- Tangazo -
MwanaSayansi
MwanaSayansihttps://sayansi.medicopress.mediai
MwanaSayansi ni chanzo mahususi cha habari, maoni na uchambuzi kuhusu sayansi na teknolojia nchini Tanzania; hasa katika nyanja ya maendeleo. Taarifa zote na maudhui huzingatia sera na taratibu za MedicoPRESS, asasi iliyoanzishwa kwa lengo la kukuza ujuzi wa waandishi wa habari na wanasayansi katika kuwasilisha taarifa za kitabibu na kisayansi kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -