- Tangazo -
Home Maoni ya MwanaSayansi Sayansi kuhusu kifo cha ghafla wakati wa kujamiiana

Sayansi kuhusu kifo cha ghafla wakati wa kujamiiana

- Tangazo -

Hivi karibuni, habari za wanaume hasa wazee kufariki wakiwa faragha na ‘wapenzi wao’ zimeteka vyombo vya habari nchini. Swala hili pia limekuwa sehemu ya mjadala kwenye mitandao ya kijamii na wengi wakilizungumza kwa mzaha.

Hatahivyo, huenda kuna wengi bado wanajiuliza: Kwanini hatari hii imeonekana kutokea zaidi miongoni mwa wazee, tena wa kiume?

Swali la msingi zaidi linaweza kuwa: Je, sayansi inasemaje kuhusu hali hii? Ni jambo la bahati mbaya au lina sababu?

Kwanza kabisa, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa hali hii haitokei kwa bahati mbaya, bali kuna  ufanano wa tabia na visababishi baina ya matukio haya.

Kifo cha namna hii hutokea kwa nadra sana. Kikitokea, mara nyingi muhanga ni mwanaume ambaye amechepuka katika ndoa yake. Sababu ya kifo mara nyingi ni tatizo kwenye mfumo wa utendaji kazi wa moyo na mishipa ya damu.

Kabla yakuchambua utafiti huo kwa undani, ni muhimu kuelewa kwamba kujamiiana ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na tendo hili likifanywa katika hali ya kawaida huwa ni salama.

Pia, kujamiiana huambatana na mabadiliko ya kawaida katika utendaji kazi wa mwili (fiziolojia), ikiwemo kufurika kwa vichocheo mbalimbali katika damu. Hali hii huambatana na kupanda kwa shinikizo la damu na mapigo ya moyo. Kwa kila dakika, mapigo ya moyo yanaweza  kuwa zaidi ya 100. Hali hii ni sawa na kufanya mazoezi juu ya wastani.

Mtu mwenye afya njema huwa haathiriki kutokana na mabadiliko haya ya mwili wakati wa kujamiiana. Lakini kwa mtu mwenye tatizo la kiafya, kwa mfano ugonjwa wa moyo, kuna mambo kadhaa yakuangalia.

Kuna baadhi ya wagojwa, haswa wazee, wanaweza kuwa wanapata ugumu kufikia mshindo wakati wa kujamiiana; kwasababu za kiafya au za kimihemko. Katika kujaribu kufikia mshindo, inawezekana watu hawa wakatumia nguvu nyingi na hivyo kuufanya mfumo wao wa moyo na mishipa kuzidiwa katika utendaji. Watafiti wanazidi kuchunguza huu mchakato kwa undani zaidi.

Hivyo, ni muhimu kwa watu walioko katika kundi hili kuchukua tahadhari kubwa. Wanashauriwa kuzungumza na madaktari wao kuhusu namna salama ya kujamiiana.

Wapo wanaotumia dawa za kuongeza nguvu. Ni muhimu kuchukua tahadhari juu ya matumizi ya dawa hizi kwani mtu  hatakiwi kuzitumia bila kumuuliza daktari kama ni salama kwake au la.

Je, kuna uhusiano na kuchepuka kwenye ndoa?

Kuna utafiti ulibaini kuwa jumla ya vifo 34 vya wanaume vilitokea wakati wakujamiiana na 80% kati ya watu hao walifariki huku wakichepuka; na sababu kuu ya kifo ilikuwa ni hitilafu katika moyo na mfumo wa mzunguko wa damu. Utafiti huu ulifanywa na madaktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa na vifo (wanapatholojia) nchini Japan.

Matokeo ya utafitu huo kutoka Japan yanaungwa mkono na tafiti nyingine zilizofanyika Korea ya Kusini ambapo madaktari walichunguza kitaalamu mfululizo wa vifo 14 vilivyotokea kwa wanaume wakati wa kujamiiana. Ilionekana ni mwanaume mmoja tu aliyefariki akifanya mapenzi na mke wake wa ndoa. Wengine wote walikuwa wamechepuka. Sababu ya kifo ilikuwa ni matatizo ya moyo. Utafiti mwingine nchini Ujerumani umeonyesha matokeo yanayoendana na haya.

Vipi kuhusu Afrika?

Katika bara la Afrika, tafiti zinaonyesha kuwa matukio haya yanapotokea mara nyingi watu hupenda kuyahusisha na imani za kishirikina, pia mwanamke hunyooshewa kidole hata kabla ya uchunguzi wa kina kufanyika.

Tafiti hizi, kama zilivyo tafiti nyingine nje ya Afrika, zimeonyesha kuwa vifo vinavyotokea wakati wa tendo la ndoa hutokea zaidi kwa wanaume wazee ambao mara nyingi huwa wamechepuka nje ya ndoa.

Kwa undani zaidi, kuna visababishi vinavyotokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ndani ya ubongo. Wahanga wake wengi walikutwa na tatizo la kuwa na shinikizo la juu la damu pamoja na kuwa na kuta dhaifu za mishipa ya damu.

Watafiti bado wanachunguza kwa undani kwanini vifo hivi hutokea zaidi kwa wanaume wenye umri mkubwa wanaochepuka  na kuliko mwanaume anayefanya tendo la ndoa na mke halali wa ndoa.

Lakini watafiti wametoa nadharia mbalimbali ikiwemo kuwa mwanaume anayechepuka huwa katika msongo mkubwa kimawazo na kimwili kwa ujumla, hali ambayo hubadilisha fiziolojia ya mwili ikiwemo shinikizo la damu kupanda, mapigo ya moyo kuwa juu vilevile wazee hujiweka katika msongo mwingine mkubwa wa kutafuta nguvu za kuwaridhisha wanawake wengine(hasa wasichana) tofauti na wanapokuwa na wake wa ndoa.

Imebainika pia katika tafiti mbali mbali kwamba wazee hutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo zinaweza kuingiliana na dawa za ugonjwa wa moyo na dawa hizi  zinaweza kushusha shinikizo la damu ghafla hadi viwango vya chini kabisa na hivyo kupelekea kifo.

Imehaririwa kwa kuzingatia sera ya uhariri ya MedicoPRESS.

Rejea

https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5479331/

- Tangazo -
Dkt Norman Jonas
Dkt Norman Jonashttp://www.sayansi.africa
Medical Doctor | Internal Medicine - Kilimanjaro Christian Medical University College | Health Communication
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -
  1. Hi,Dr Norman Jonas,I real appreciate your report on this matter of sudden death especially to the old men, You have made this matter very clear that every one is now aware of the reason why …..and what should be done to avoid this matter ,however, some of the people connect this with superstitions acts and some go far to freemason believes but today you have made it so clear and society should now understand what is the cause of all these and what are the measure to be followed to avoid it.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -