- Tangazo -
Home Maoni ya MwanaSayansi Njia za kuimarisha kinga yako dhidi ya maambukizi

Njia za kuimarisha kinga yako dhidi ya maambukizi

- Tangazo -

Kama uko katika mazingira yanayokuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi ya vimelea, vikiwemo virusi vya korona au hata bakteria, silaha yako ya kwanza ni kujiweka salama kwa kuzingatia kanuni za afya. Vaa barakoa, nawa mikono kwa sabuni na maji tiririka au tumia vitakasa mikono.

Lakini ikitokea ukapata maambukizi, moja ya vitu vitakavyoamua uponaji wako ni uimara wa mfumo wako wa kinga katika kukabiliana na maambukizi hayo.

Watu wengi mawekuwa wakiuliza swali: Je, nawezaje kuimarisha kinga yangu ya mwili dhidi ya maambukizi?

Ushahidi wa kisayansi umebaini mbinu mbalimbali zinazoweza kukusaidia na umetoa majibu ya maswali maalum kama ifuatavyo:

Lishe ina uhusiano gani na mfumo wa kinga?

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya uimara wa mfumo wa kinga na ubora wa lishe ya mtu hasa kwa kundi la wazee. Uhusiano huu unaweza kujengwa katika njia mbalimbali.

  • Kwanza kabisa, fahamu kwamba seli hai za mwili wako ndizo hupambana dhidi ya vimelea pale vinapokuvamia. Seli hizi ni sehemu ya mfumo wako wa kinga na huitaji nishati ya uhakika katika ufanyaji kazi.
  • Pili, mwili unahitaji virutubisho muda wote ili kutengeneza protini za kinga ambazo huangamiza vimelea vamizi.
  • Tatu, virutubisho aina ya madini lishe na vitamini uhitajika zaidi ili kuwezesha mfumo wa kinga katika kujenga kile kiitwacho mfumo tata (antioxidant defense mechanism) ambao ni muhimu sana katika kupunguza athari za uharibifu wa maambukizi hasa ya virusi katika tishu za mwili.

Hivyo ni muhimu kufahamu kuwa mfumo bora wa kinga hujengwa na lishe bora. Tafiti zimeonyesha kuwa watu ambao wana ulaji mbovu hukabiliwa na matatizo yakiafya, yakiwemo utapiamlo na mfumo dhaifu wa kinga. Ili kupata virutubisho muhimu kwa mfumo kinga ni muhimu kuwa na ulaji sahihi; hasa wa vyakula vyenye vitamini na madini lishe kwa wingi. Hili linajumuisha mboga za majani, matunda, nafaka kama maharagwe, samaki n.k, wakati huo kupunguza vinywaji kama soda na pombe.

Mazoezi je?

Kuna ushahidi unaojitosheleza kisayansi kuwa mfumo wa kinga huitikia kutokana na mazoezi ya mwili ya mara kwa mara. Mwitikio huu hutegemea kiwango cha mazoezi. Tafiti ziimeonyesha kuwa mazoezi ya kiwango cha wastani hadi juu kwa muda wa dakika 60 husisimua na kuamsha utendaji kazi wa seli maalumu za kinga pia huboresha mzunguko wa protini maalumu za mfumo wa kinga ziitwazo kwa kitaalam antibodies na cytokines.

Mazoezi huboresha mzunguko wa damu katika kila tishu ya mwili wako, hivyo husaidia pia seli za kinga ya mwili kufanya doria ya kugundua na kuondoa vilimelea vya magonjwa. Jambo muhimu la kufamu ni kwamba hauhitaji kwenda gym na kunyanyua vyuma vizito ili kuhesabika umefanya mazoezi bali hata kutembea kwa kasi , kuruka kamba ni sehemu ya mazoezi ya mwili. Ili kupata faida za mazoezi ni muhimu kufanya mazoezi walau mara 5 kwa wiki kwa wastani wa dakika 30 kwa kila siku.

Usingizi wa kutosha unachangia?   

Ndiyo. Usingizi ni kitu muhimu sana katika utendaji kazi wa mwili, afya na uhai wa kila mwanadamu. Mwili hutumia usingizi kuleta usawaziko katika utendaji kazi wa mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo kinga wa mwili. Tafiti zinaonyesha kuwa tunapolala, mwili hutumia usingizi kufanya uponyaji wa tishu za mwili .Kutopata usingizi wa kutosha kwa muda mrefu hudhoofisha utendaji kazi wa mfumo kinga wa mwili.  Watu wanaolala chini ya masaa 6 kwa siku huwa na mfumo kinga dhaifu na kuwa na uwezekano wa kuugua mara kwa mara na magonjwa kama mafua, kikohozi na marahi mengine. Pia tafiti zinaonyesha kuwa kutolala kwa muda wa kutosha huchangia kuongeza hatari ya magonjwa mengine  kama kisukari na unene uliokithiri.

Msongo wa mawazo na kinga ya mwili

Kipindi cha mlipuko wa magonjwa, kama ilivyo katika janga la virusi vya korona(UVIKO-19), kiwango cha msongo wa mawazo kwa watu wengi huwa juu. Vilevile msongo huweza kuchangiwa na sababu mbalimbali kama matatizo kazini, kwenye mahusiano au ukata wa fedha. Msongo wa muda mrefu hudhoofisha kinga ya mwili na kupunguza uwezo wa mwili kupambana na magonjwa. Mtu aliye kwenye msongo mkubwa wa mawazo kwa muda mrefu hukabiliwa na hatari ya kuugua mara kwa mara ikiwemo magonjwa kama mafuta, maambukizi ya virusi pia kuongeza uwezekano wa magonjwa kama ya moyo na mishipa ya damu, kisukari n.k. Hivyo ni muhimu kujenga mazoea ya kupumzisha akili kama kujumuika na kufurahi na marafiki hata ikiwezekana kupata likizo. Ukiwa na msongo wa mawazo, usikae kimya, shirikisha mwenzako unayemwamini. Kukaa kimya na kujitenga huzidisha msongo huo.

Kinga ya mwili na umri

Kadri tunavyozeeka, uwezo wa miili yetu kupambana na maradhi hupungua pia. Wazee wana uwezekano mkubwa wa kushambuliwa na vimelea vya maradhi kuliko vijana. Ushahidi unaweza kuonekana dhahiri kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya korona kwa wazee, ambao wako katika hatari zaidi ya kuugua dalili mbaya kuliko vijana. Hivyo, ni muhimu kwa watu wenye umri mkubwa kuchukua hatua zaidi kujikinga na maradhi mbalimbali kwa kuzingatia kanuni za afya.

Chanjo na kinga ya mwili

Chanjo ni kitendo cha kusisimua kinga ya mwili kutengeneza ulinzi dhidi uvamizi wa vimelela wa magonjwa. Hii hufanyika kwa kuingiza mwilini molekyuli ambazo husisimua mwitikio wa mwili.  Mwitikio huu huacha kukumbukumbu ya kinga,  hivyo mwili huwa na uwezo wa kujikinga haraka endapo itatokea utakutana na kimelea wa magonjwa mwenye ufanano na molekyuli za chanjo. Chanjo ni moja ya ugunduzi bora kuwahi kutokea katika historia ya sayansi ya tiba. Takwimu zinaonyesha kuwa chanjo inasadia kuepusha vifo milioni 2 hadi 3 kwa mwaka. Shirika la afya duniani linalipoti kuwa kwa sasa magojwa zaidi ya 23 yanakingwa na chanjo.

Soma zaidi: Chanjo dhidi ya korona: Fahamu mchakato wa uvumbuzi, majaribio na matumizi

Mfano ni ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao iwapo ukimpata mtu uwezekano wa kupona ni mdogo na vifo hufikia hadi 100% lakini hukingwa na chanjo ya kichaa cha mbwa iwapo umeng’atwa. Ugonjwa mwingine ni ugonjwa wa pepopunda (tetanus) ambao matokeo yake si mazuri kwa wahanga wengi lakini chanjo husaidia kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya vimelea wa tetanus.

Baadhi ya magonjwa makubwa mengine yaliyo na chanjo ni pamoja na chanjo dhidi ya virusi vya HPV ambavyo husababisha saratani ya shingo ya kizazi na koo, ugonjwa wa dondakoo, homa ya ini aina aina B, surua, homa ya mapafu, ugonjwa wa kuhara unaotokana na virusi vya Rota, homa ya manjano, ugonjwa wa kupooza wa polio, homa ya mapafu. Chanjo za baadhi ya magonjwa bado zipo katika hatua mbalimbali za utafiti ikiwemo chanjo za UKIMWI na malaria. Aina ya chanjo inayotolewa hutegemea na sera za nchi hasa kuangalia kulinda  makundi yaliyo katika hatari ya kupata ugonjwa flani.

Mwisho, ili kujikinga na maradhi mbalimbali ni muhimu kuzingatia kanuni za afya ikiwemo usafi wa mazingira, matumizi sahihi ya vyoo bora, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kupata chanjo kwa baadhi ya magonjwa yenye chanjo , kuzingatia kanuni za kujikinga na maradhi yanayoenezwa kwa njia ya ngono isiyo salama kama VVU na magonjwa ya zinaa.

- Tangazo -
Dkt Norman Jonas
Dkt Norman Jonashttp://www.sayansi.africa
Medical Doctor | Internal Medicine - Kilimanjaro Christian Medical University College | Health Communication
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -