- Tangazo -
Home Maoni ya MwanaSayansi Mwelekeo wa Tanzania, Afrika katika upatikanaji wa tiba ya ‘sikoseli’

Mwelekeo wa Tanzania, Afrika katika upatikanaji wa tiba ya ‘sikoseli’

- Tangazo -

Kuna uhitaji wa haraka wa mkakati wa tiba za ugonjwa wa sikoseli (selimundu) barani Africa, hatahivyo, hapa nchini Tanzania kuna mambo kadhaa yakujifunza kuhusu juhudi za uwekezaji katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

Sikoseli ni ugonjwa unaosababisha seli nyekundu za damu kuwa na umbo lisilo la kawaida; mfano wa mundu au mwezi mchanga. Mtu mwenye sikoseli anakuwa amerithi vinasaba vyenye hitilafu katika chembe za hemoglobin ambazo hutengeneza seli nyekundu za damu.

Katika bara la Africa, na hususani hapa Tanzania, sikoseli ni ugonjwa unaopaswa kutiliwa mkazo katika afua za afya ya jamii.  Hivyo, ni muhimu kuwa na mkakati utakaowezesha upatikanaji wa uwanja mpana wa tiba za ugonjwa huu.

Inakadiriwa kuwa kati ya mwaka 2010 hadi 2050 watoto milioni 14 duniani, wamezaliwa/watazaliwa wakiwa wamerithi sikoseli na kati ya hao, 84% wanatoka Afrika.

Pia katika vifo, uwezekano wa mgonjwa wa sikoseli kusalimika hapa Afrika ni mdogo lakini afua stahiki zikizingatiwa, uwezekano wa watoto wenye huu ugonjwa kuishi unaweza kuongezeka na kufikia kati ya 50% na 90%.

Kwingineko duniani

Kuna afua mbalimbali ambazo zimewezesha watoto kunusurika na ugonjwa wa sikoseli katika nchi kama Marekani, Uingereza na kwingineko, mathalani  utambuzi wa mapema wa waathirika wa ugonjwa; hasa upimaji wa watoto wachanga, uingizwaji wa wagonjwa wa sikoseli katia huduma kamili zinazohusisha kuzuia maambukizi mengine na kutibu haraka madhara ya siko seli.

Iwapo afua hizi zitatumika kikamilifu inawezekana kupandisha kiwango cha watoto wenye sikoseli wanaonusurika vifo hadi asilimia 50 lakini, ili kufikia 90%  afua mahususi kwa ugonjwa wa sikoseli zinahitajika.

Kwa Tanzania, takribani watoto 11,000 huzaliwa wakiwa na sikoseli kila mwaka na kulingana na utafiti wa Modell na Darlison, magonjwa ya jamii ya sikoseli huchangia hadi 3.4% ya vifo vya watoto chini ya miaka 5 dunia nzima. Inakadiriwa kila mwaka, vifo vya watoto wachanga ni kati ya 70 hadi 80 kwa kila vizazi hai 1000.

Tumetoka wapi?

Tanzania ina kliniki maalumu ya sikoseli; ya kwanza, katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilianzishwa mwaka 1980. Pia, Wizara ya Afya ilikuwa na sera ya kuwapa msamaha wa malipo  wagonjwa wa sikoseli wanaohudumiwa hospitali za umma.

Mwaka 2004, chuo kikuu cha Afya na Sayasi shirikishi Muhimbili(MUHAS) kilianzisha mradi wa utafiti uliohusisha kutoa huduma za afya, uhamasishaji wa kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa sikoseli pia kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya na wanasayansi.   Mradi huu wa sikoseli umepanua wigo na kuanza kutoa huduma katika hospitali nyingine za mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza.

Katika kupanua wigo wa utoaji huduma za sikoseli, mradi huu umefanya kazi na wizara ya afya kutengeneza mwongozo wa utoaji tiba za sikoseli katika ngazi mbalimbali za vituo vya afya.

Mwongozo huu umeunganishwa kwenye mpango mkakati wa taifa wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambao unaendana na mwongozo wa shirika la afya duniani(WHO) kuhusu magonjwa yasiyoambukiza katika bara la Africa.

Pamoja na kuwapo kwa mwongozo huu, kuna changamoto ya upatikanaji  wa gharama nafuu kwa dawa aina ya hydroxyurea. Nchi kama Ghana zimechukua jukumu la kushirikiana na kampuni ya dawa ya Novartis kusaidia upatikanaji wa dawa (https://www.novartis.com/global-health/sickle-cell-disease) pia Nigeria inazalisha dawa ya hydroxyurea ndani ya nchi.

Tiba hapa nchini

Tanzania imefanya juhudi kuhusu upatikanaji wa dawa hizi ndani ya nchi. Mradi wenye lengo la kuzalisha dawa za hydroxyurea ndani ya nchi umepatiwa idhini na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na utasaidia dawa hizi kupatikana kwa gharama ndogo na kwa wepesi.

Nchi nyingi Afrika zimetamani sana kuhakikisha huduma za msingi kwa wagonjwa wa sikoseli zinapatikana kabla ya kuanzisha huduma ya upandikizaji  seli shina za damu (haematopoietic stem cell transplantation). Lakini kuna sababu kadhaa zimeongeza kasi katika utafutaji wa tiba za sikoseli.

Kwanza kumekuwepo na hatua chanya katika uwanda wa upandikizaji hasa kwenye maboresho ya mbinu bora zenye matokeo mazuri zaidi . Pili,  kumekuwepo na ongezeko la uhitaji kwa wagonjwa wa sikoseli kupata tiba ya upandikizaji wa selishina, baadhi wameamua kwenda kutafuta tiba nje ya bara la Afrika kama India , Canada na Marekani.

Tatu, nchi za Afrika zimefanya uwekezaji mkubwa katika huduma za kibingwa za tiba, hii inachochea uanzishwaji wa huduma ya upandikizwaji selishina ndani ya Afrika. Kwa matokeo hayo, Tanzania imeanza kuhudhuria makongamano na mikutano inayohusu tiba za sikoseli (Upandikizaji selishina na tiba ya vinasaba).

Mikutano hii inahusisha mkutano wa Regensburg, Ujerumani, mwaka 2015 na 2017. Hii ilifuatiwa na kuanzishwa kwa mkakati wa pamoja kati ya Wizara ya Afya na wadau kutoka Italy ili kusaidia uanzishwaji wa huduma za kupandikiza selishina nchini (http://www.cure2children.org/).

Mwaka 2018, Tanzani iliandaa kozi maalumu kuhusu maendeleo ya sayansi ya tiba ya magonjwa ya damu ambayo ilihusisha wadau wa tiba ya upandikizaji selishina kutoka ulimwenguni kote (https://www.en.fondazione-menarini.it/Home/Events/Advances-in-Haematology-in-Africa/Presentation).

Maswali muhimu kuhusu upandikizaji

Kuna maswali muhimu yanayohitaji kujibiwa. Je, huduma za upandikizaji selishina zitakuwa zinafanyika wapi ndani ya Tanzania? Nani atatoa huduma hizo? Namna gani huduma hizi zitatolewa? Gharama zitakuwaje? Je wazazi watakuwa tayari watoto wao kufanyiwa upandikizaji? Majibu kwa baadhi ya maswali haya yatasaidia kutoa mwongozo wa kusaidia kuanzishwa kwa huduma hizi nchini. Juhudi za kuanzishwa kwa huduma hizi zitahitaji muunganiko wa huduma za afya, uhamasishaji, tafiti na mafunzo.

Kuhusu Utoaji huduma za afya, hospitali za kibingwa nne nchini zimeonekana zina miundombinu na rasilimali ambayo inaweza kuboreshwa na kuweza kutoa huduma ya upandikizaji selishina. Hospitali tatu ni za umma ambazo ni Hospitali ya taifa Muhimbili – Upanga, Hospitali ya taifa Muhimbili – Mloganzila(http://www.mnh.or.tz/); Hospitali ya Benjamin  Mkapa iliyopo Dodoma (https://health.eac.int/institutions/benjamin-mkapa-hospital-dodoma).  Pia kuna hospitali ya rufaa ya kanda ya ziwa inayoendeshwa na Kanisa Katoliki, Hospitali ya Bugando – Mwanza (https://www.bugandomedicalcentre.go.tz/). Hospitali ya Aga Khan Hospital – Dar-es-Salaam ni hospitali nyingine binafsi iliyoonekana kuwa na huu uwezo (https://www.agakhanhospitals.org/DarEsSalaam).

Mwaka 2017, ripoti za kitabibu zilionyesha kuwa tiba ya vinasaba imefanikiwa kutibu sikoseli nchini Ufaransa hivyo kuongeza hali ya hamasa na shauku kwa jamii, wadau na serikali katika juhudi za kuanzisha huduma ya kutibu sikoseli nchini.

Tiba ya vinasaba Tanzania

Tanzania inaweza kufikiria tiba ya vinasaba kama sehemu ya mkakati wa kutibu sikoseli. Hii ni kwa sababu miundominu na rasilimali ya tiba ya vinasaba na tiba ya upandikizaji seli shina vinarandana. Zaidi, tiba ya vinasaba ina faida zaidi ya tiba ya upandikizaji kwa sababu huitaji mtu wa kujitolea lakini ni muhimu kufahamu kuwa tiba ya vinasaba bado ipo katika hatua za kitafiti ilhali tiba ya upandikizaji imethibitishwa tayari.

Hasara za muda mrefu za tiba ya vinasaba bado hazijafahamika. Kuna hatua zinapigwa katika maendeleo ya tafiti za vinasaba ndani ya Afrika ambazo zinasaidia kuelewa ugonjwa wa sikoseli kiundani hasa kuhusu vinasaba na mazingira, ambazo zitasaidia kuja na mipango mikakati inayoendana na mazingira.

Tiba ya ugonjwa wa sikoseli inahitaji wataalamu wabobezi wenye ujuzi wa kutosha katika nyanja za kutibu na maabara. Tanzania imefanikiwa kuanzisha kozi ya ubobezi ya tiba ya magonjwa ya damu ambayo inachukua miaka 3 kama shahada ya uzamili katika tiba na miaka miwili kama shahada ya uzamivu  katika sayansi ya tiba. Pia kuna kozi za wauguzi, wataalamu wa maabara na wataalamu wengine wa sayansi shirikishi.

Zipo kozi fupi na kozi za uzoefu kazini ambazo hutolewa kwa wataalamu wazawa pia wataalamu wakitanzania husafiri nje ya nchi ili kujifunza na kupata uzoefu hasa Uingereza na Marekani  (http://stage.hematology.org/Global/204.aspx) na http://www.glocalfellows.org/international/Pages/Tanzania.aspx.

Mshikamano ni nyenzo kuu

Uhamasishaji kuhusu ugonjwa wa sikoseli unafanywa kwa ushirikiano na asasi na vikundi vya kijamii. Kuna jumuiya ya vijana wanaopambana na sikoseli, jumuiya ya watu wanaoishi na siko seli, kupitia ushirikiano huu juhudi za uhamasishaji zinafanyika kwa kampeni za kijamii, kampeni za kujitolea damu, na kuuandaa shughuli za maadhimisho ya siku ya sikoseli kila mwaka inayosherehekewa Juni 19.

Shughuli za uhamasishaji zinahusisha makundi madogo katika jamii hadi ngazi za juu za kiserikali. Hii imekuwa nyenzo muhimu katika upatikanaji wa rasilimali za kuboresha utoaji huduma za afya, uhamasishaji, tafiti na ufundishaji.

Tanzania imeonyesha mfano kuwa kuna matumaini ya upatikanaji wa huduma za kutibu sikoseli lakini msisitizo umewekwa kuhakikisha huduma za msingi za sikoseli zinapatikana kwa wagonjwa wote.

Njia inayoonyesha mafanikio katika kufikia lengo ni ujumuishi wa huduma za afya, uhamasishaji, tafiti na mafunzo. Kiungo muhimu katika kufanikisha hili ni ushirikiano kati ya wadau na serikali ndani na nje ya Tanzania.

Makala haya yametafsiriwa na Dk Norman Jonas kutoka katika andiko la Professa Julie Makani: https://www.sciencedirect.com/science/article/pii/S1658387620300388 kwa niaba ya Mpango wa Siko Seli-Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.

- Tangazo -
Avatar
Prof Julie Makani
Julie Makani (born 1970) is a Tanzanian medical researcher. From 2014 she is Wellcome Trust Research Fellow and Associate Professor in the Department of Haematology and Blood Transfusion at the Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS). Also a visiting fellow and consultant to the Nuffield Department of Medicine, University of Oxford, she is based in Dar es Salaam, Tanzania. In 2011, she received the Royal Society Pfizer Award for her work with sickle cell disease.
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -