- Tangazo -
Home Maoni ya MwanaSayansi Mikutano ya kidigitali wakati wa korona, changamoto kwa nchi za Afrika na...

Mikutano ya kidigitali wakati wa korona, changamoto kwa nchi za Afrika na mustakabali

- Tangazo -

Mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) duniani na hususani barani Afrika, umeleta changamoto nyingi kwenye sekta ya elimu kutokana na zuio la mikusanyiko ya watu.   Dunia imelazimika kugeukia njia za digitali ili kuendeleza shughuli za mwasiliano na elimu, ikiwemo mikutano na semina za wanataaluma mbalimbali wakiwemo wanasanyansi.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika na kwingineko, Tanzania imefuata mkondo huu wa kutumia majukwaa mbalimbali ya kuwasiliana kwa njia ya mtandao kwenye mafunzo mafupi, semina na mikutano ya kitaaluma. Baadhi ya majukwaa maarufu yanayotumika kwenye mikutano kwa njia ya mtandao ni Zoom, Skype, GoToMeetings, Microsoft Teams, na Google Hangouts.  

Majukwaa haya yamesaidia kwa kiasi kikubwa;  hata hivyo,  haikua rahisi kuandaa na kushiriki matukio mbalimbali kwanjia hii. Changamoto mbalimbali zilijitokeza, hasa kwa nchi za Afrika.

Japokuwa changamoto hizi za mawasiliano kutokana na janga la UVIKO-19 ziliwakabili waandaji na washiriki wa mikutano ya kidigitali duniani kote, hapa tunaangazia zaidi changamoto tulizokabiliana nazo ndani ya Tanzania; ambazo zinaweza kufanana kwa kiasi kikubwa na nchi nyingine za Afrika.

Pia, tunatoa dondoo na ushauri kuhusu njia bora za kuendesha matukio kwa njia ya digitali katika mazingira ya Afrika kutokana na uzoefu tulioupata wakati wa kuandaa, kuendesha na kushiriki shughuli za kidigitali kama wanasayansi chipukizi. Ni matumaini yetu kwamba  dondoo hizi na uzoefu zitasaidia waandaaji na washiriki wengine kuendesha mafunzo na mikutano ya kidijitali yenye tija zaidi.

Changamoto kwenye kuandaa na kuendesha shughuli 

Kwa upande wa waandaaji, moja ya changamoto kubwa zaidi ni gharama kubwa za mtandao wa intaneti na uwezo hafifu. Kasi ya intaneti katika nchi nyingi za Afrika ipo chini kulinganisha  na maeneo mengine duniani. Pia, ni kawaida kwa upatikanaji wa huduma ya intaneti kubadilika mara kwa mara kutegemeana na mahali mtumiaji alipo. Hii inapelekea mtandano kukatika mara kwa mara wakati shughuli zikiendelea na kuwaaacha washiriki njia panda.

Kukabiliana na hili, ni muhimu kuwa na mbadala (backup) wa chanzo cha intaneti wakati wote. Kwa Tanzania, hii inamaanisha kununua vifurushi vya intaneti kutoka zaidi ya mtandao mmoja. Ikiwezekana, mtaalamu wa mawasiliano (IT personnel) awepo tayari  kushughulikia changamoto zozote za kimtandao zitakazojitokeza.

Ni muhimu pia kwa waandaaji  kujiweka tayari kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza, kwa  kufanya mazoezi ya kurusha semina au mkutano pamoja na wawezeshaji kabla ya siku ya tukio.

Tukiangalia mbele, mafunzo na mikutano kwa njia za digitali huenda vikabaki hata baada ya UVIKO-19 kudhibitiwa. Hivyo, ni muhimu kutafuta namna za kuendesha shughuli hizi kwa ufanisi zaidi licha ya changamoto zilizopo. Kufanikisha hili, tunashauri  kutumia taasisi/kampuni zenye uhakika wa intaneti kama kitovu cha kuwakutanisha washiriki na kujiunga na mafunzo kwa intaneti kwa pamoja. Muundo huu umeanza kutumika kitambo kidogo barani Afrika na mfano mzuri ni kozi fupi za digitali ‘bioinformatics’ (Introduction to Bioinformatics (IBT) course) zinazoendeshwa na H3ABioNet  kila mwaka  tangu mwaka 2016 kwa mafanikio makubwa na kuwafikia washiriki wengi barani Afrika. Mpangilio huu unaweza kuongeza washiriki na umependekezwa kama mbadala wa mikutano ya ana kwa ana.

Changamoto nyingine itokanayo na mikutano ya kidigitali ni mahudhurio hafifu hata pale ambapo wanaojisajili ni wengi. Uzoefu wetu wa kuandaa mikutano na mafunzo ya kisayansi kwa njia ya mtandao umetuonyesha kwamba baada ya kufanya matangazo ya kutosha  mwitikio huwa ni mzuri na watu hujisajili, hata kuzidi kiwango cha watu waliotegemewa. Hata hivyo, wahudhuriaji  huwa ni wachache, takribani asilimia 25 – 50 ya waliojiandikisha. Na kwa wanaojiunga ni wachache tu hubaki zaidi ya saa moja au hadi mwisho wa mkutano/kipindi.

Changamoto hii inaweza kusabibishwa na matatizo ya mtandao au wahudhuriaji wenyewe, pamoja na sababu nyinginezo. Tulijifunza kwamba kufadhili wahudhuriaji wa mikutano/vipindi hivi kwa kuwapa nyenzo za kusaidia mawasiliano kama vifurushi vya intaneti kunaongeza idadi ya washiriki wa mikutano au mihadhara kwa njia ya mtandao. Hii inatakiwa kwenda bega kwa bega na ufuatiliaji wa waalikwa/waliojiandikisha ikiwemo kukumbushana kwa njia ya ujumbe wa simu   au kwa kupiga simu kabisa.

Kuliko kutuma barua pepe, kutuma ujumbe na kupiga simu vimeonyesha   ufanisi zaidi, labda kwa sababu wengi hawatumii au kuangalia barua pepe mara kwa mara kama simu ya mkononi. Pia, njia hizi hazihitaji kuwa na intaneti, ambayo kama tulivyoeleza awali, haipatikani kwa urahisi kwa watu wengi katika ukanda huu wa Afrika

Kwa kuongezea, ni muhimu kwa waandaaji kutuma miongozo ya namna ya mkutano utakavyofanyika na namna ya kutumia jukwaa litakalotumika walau mara mbili kabla ya tukio. Tunashauri pia waandaaji kusajili watu wengi mara dufu zaidi ya washiriki wanaowategemea/wanaoweza kuwawezesha ili kuhakikisha idadi inayotegemewa inafikiwa.

Uendelevu wa mikutano ya kidigitali pia unasua sua, hasa kutokana na ukosefu wa udhanimi wa gharama za uendeshaji ukilinganisha na warsha na mikutano ya ana kwa ana. Warsha na mikutano ya ana kwa ana imezoeleka na tayari gharama zake zinajulikana. Mabadiliko ya ghafla kwenda digitali imewaacha waandaji pamoja na wadhamini gizani. Hii ni kwa sababu mahitaji na gharama zake havipo wazi sana na vinaenda vikibadilika kila mara. Pia, wadhamini mara nyingi hua wanapata faida ya kujitangaza na kufikisha ujumbe wa taasisi au kampuni zao kwa kupitia mikutano, warsha na semina wanazodhamini. Kwa matukio ya kwenye mtandao, hili haliko wazi ni kwa namna gani linaweza kufanikiwa, hivyo kupunguza motisha wa kudhamini shughuli hizi.

Waandaji wanashauriwa kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya udhamini na kuwa wabunifu kwenye namna za kushirikiana na wadhamini. Njia nyingine ni kushirikiana na kuunganisha juhudi na washirika wengine wanaofanya shughuli zinazofanana ili kupunguza gharama na kuboresha ufanisi.

Changamoto kwa washiriki 

Kwa upande wa wahudhuriaji, uelewa mdogo  kuhusu jinsi mikutano kwa njia ya mtandao inavyofanyika limekua ni tatizo kubwa,  mathalani namna ya kutumia kamera, vinasa sauti, vyumba vya majadiliano na vinginezyo. Ndani ya Tanzania, kama sehemu nyingine Afrika, mikutano na elimu kwa mtandao vilikuwa havijashika kasi kabla ya mlipuko wa UVIKO-19. Lakini sasa tumelazimika kujifunza na kubadilika kwa haraka. Hivyo, hili linaweza kuchukua muda kidogo kubadilika.

Wakati mwingine mikutano ya mtandaoni hugeuka  kuwa yenye kelele nyingi na kutosikilizana, jambo ambalo linachangia sana kupoteza muda na umakini. Ni muhimu kwa waandaaji kuwa makini muda wote na kuchukua hatua kama vile kuzima vinasa sauti vya washiriki wanaoleta changamoto na vilevile kuondoa baadhi ya watu kweye shughuli.

Namna nyingine ya kukabiliana na hili ni kwa washiriki kujifunza na kuelewa namna majukwaa mbalimbali ya mikutano kwa njia ya mtandao yanavyofanya kazi. Waandaaji wana jukumu pia la kuwapa washiriki maelezo na miongozo iliyokamilika kabla na wakati wa tukio. Pia, tunawashauri washiriki na wao kuwa na mbadala wa huduma ya intaneti na vifaa vyenye chaji ya kutosha ili iwapo mtandao au umeme utakatika, wawe na mbadala.

Hitimisho

Majukwaa ya kidigitali yametuwezesha kuendelea na mawasiliano, mikutano na mafunzo licha ya kua na vikwazo vingi vilivyotokana na homa janga la UVIKO-19. Majukwaa haya ya kimtandao ni mapya na yamekuja na changamoto zake, hasa kwa Tanzania na nchi za Afrika. Ni jambo la muhimu kwa wandaaji ni kuchagua jukwaa ambalo linafaa kwa mazingira na maudhui yao wakitilia maanani umaarufu, urahisi wa kutumia na matumizi ya vifurushi vya intaneti. Kwa mfano,  ni rahisi kuandaa mkutano kwenye jukwaa la Zoom kwa sababu watu wengi wanaufahamu na wameshazoea kuitumia kuliko jukwaa lingine. Tunatumahi kuwa wasomaji wetu wamepata mwanga wa namna gani ya kuandaa mikutano, mafunzo, mihandara na warsha kwa njia ya mtandao na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kama tulizopitia.

Sehemu kubwa ya makala haya imechapishwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kiingereza hapa:  https://ecrlife.org/running-virtual-workshops-in-africa/ 

Waandishi washiriki ni Grantina Modern na Mohammed Zahir Mtafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili ni Dkt Norman Jonas

- Tangazo -
Avatar
Aneth Davidhttps://anethdavd.wordpress.com/
Aneth ni mwanasayansi chipukizi na mwanataaluma wa baoteknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nje ya sayansi, Aneth anajishughulisha na masuala ya uwazi kwenye sayansi na ujumuishaji.
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -