Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 kumekuwa na jitihada za pamoja barani Afrika katika kukabiliana na ugonjwa wa siko seli. Jambo lenye kuleta matumaini ni kwamba, jitihada hizi zimeanza kuonyesha mafanikio.
Kwa upande mwingine, kuna changamoto katika maeneo manne. Changamoto ya kwanza ni uwepo wa maeneo machache ya kitafiti kwaajili ya ugonjwa wa siko seli na hivyo kupelekea kuwa na tafiti chache zinazozalishwa ndani ya bara la Afrika.
Pili, hakuna uthibitisho kuwa matibabu ya siko seli hutolewa kwa usawa na kwa viwango thabiti na kila sehemu barani Afrika. Tatu, kuna uhaba mkubwa wa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha ili kukabiliana na ugonjwa huu. Mwisho, kuna miradi michache inayoshughulika na kutafiti kuhusu afua mbalimbali na kutoa miongozo ya tiba ya ugonjwa wa siko seli ndani ya bara.
Pia, si jambo geni kusikia kwamba Afrika inakabiliwa na mzigo mkubwa wa ugonjwa wa siko seli huku kukiwa na huduma hafifu za tiba dhidi ya ugonjwa huo. Wagonjwa wengi wa siko seli hawapati faida ya kugunduliwa mapema iwapo wana ugonjwa wa huo. Na wale wanaobahatika kugunduliwa mapema hawapati dawa kinga dhidi ya maambukizi aina ya Penicillin; pia dawa za kuboresha hali ya mgonjwa; aina ya hydroxyurea.
Kwa upande mwingine, changamoto hizi zimekuzwa zaidi na kuwapo kwa ushirikiano hafifu miongoni mwa wataalamu ndani ya Afrika. Ni muhimu sana kwa wataalamu kushirikishana uzoefu na kupunguza kufanya marudio katika maeneo ambayo tayari kuna jitihada dhidi ya ugonjwa wa siko seli.
Huwa ni kinyume cha maadili kufanya tafiti bila kusaidia kutatua matatizo ya utoaji huduma, hivyo ni wakati muafaka kwa watafiti, wanataaluma, watoa huduma za afya na taasisi za kitaaluma kushirikiana na sekta za umma na binafsi katika kuwekeza kwenye miongozo na sera za kisayansi zenye mashiko kwenye kutatua changamoto za ugonjwa huu.
Kwa namna ya pekee, tumeanza kuona juhudi za madaktari, wakufunzi na wanasayansi kutoka katika miradi na shughuli mbalimbali zinazohusika na udhibiti wa ugonjwa wa siko seli ndani ya Afrika, mathalani kuanzishwa kwa jumuiya ya SickleInAfrica.
Hii ni fursa muhimu sana katika mapambano dhidi ya siko seli, hasa tukizingatia kwamba jumuiya hii ilianzishwa ili kutatua changamoto zinazokabili juhudi za wataalamu kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Juhudi hizi zimeonekana kupitia maboresho ya sera na miongozo ya sekta ya afya katika nchi zinazokabiliwa na mzigo mkubwa wa ugonjwa wa siko seli.
Nchi zilizochaguliwa kuunda jumuiya hii, ikiwamo Tanzania, zina idadi kubwa ya watu wanaoishi na ugonjwa wa siko seli, zenye vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa huu lakini pia zina mwitikio mdogo katika kuhamasisha mbinu za tiba ambazo zingepunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5.
Mwamko huu wa kushughulikia tatizo la siko seli ndani ya Afrika umekuja wakati muafaka, tukizingatia kuwa kuna vuguvugu katika maendeleo na tafiti za sayansi ya vinasaba ndani ya bara la Afrika.
Jumuiya hii ya wataalamu ina miradi mikuu mitatu; kwanza ni Sickle Pan- African Research Consortium (SPARCo) ambayo ina matawi kwenye Chuo kikuu cha Afya na Sanyasi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kilichopo Tanzania, Chuo kikuu cha Abuja (Nigeria) na Chuo kikuu cha Kwame Nkurumah (Ghana).
Lengo kuu la SPARCo ni kuboresha uwezo wa tafiti za ugonjwa wa siko seli Afrika kupitia kuboresha miundombinu, elimu na ujuzi. Pia hutoa taarifa za ugonjwa wa siko seli na kutafsiri matokeo ya tafiti kwenda kwenye vitendo na utendaji.
Pili, ni Sickle Africa Data Coordination Center (SADaCC ) huu ni mradi uliopo chuo kikuu cha Cape Town, Afrika kusini. Hiki ni kituo cha kiutawala kinachohusika na kuratibu takwimu, taarifa na mawasiliano ya mradi wa SPARCO. Tatu ni Sickle Cell Pan- African Network; huu ni mtandao wa watafiti, matabibu, wakufunzi, wafadhili na vituo vinavyofanya kazi kutatua tatizo la ugonjwa wa siko seli. SPAN ina jumla ya vituo 22 katika nchi 17 ndani ya Afrika.
Kwa kipindi cha miaka 3 sasa; jumuiya hizi zimefanikiwa kuanzisha rejesta ya wagonjwa wa siko seli. Rejesta ina jumla ya wagonjwa 13,000 ambao wameunganishwa kwenye kumbukumbu za taasisi mbalimbali za afya. Kuanzia Oktoba 2018 hadi Machi 2019, wagonjwa wa siko seli 1,685 walisajiliwa kwenye rejesta sawa na 48% ya lengo ambalo ni wagojwa 1,751 (28%) kwa Ghana, 2,900 (46%) kwa Nigeria, na 1,634 (26%) kwa Tanzania.
Kupitia ushirikaino huu, tunazidi kushuhudia mafanikio katika kutengeneza miongozo ya matibabu ya ugonjwa wa siko seli. Miongozo hii inatokana na miongozo 12 iliyochapishwa ndani ya miaka 10; inajumuisha miongozo mikuu 7 (4 kutoka nchi za Afrika ambazo ni Nigeria, Tanzania, Afrika Kusini na Ghana na mingine 3 kutoka Jamaica, Marekani na Canada).
Je uwepo wa SickleInAfrica una manufaa gani?
Jumuiya hii inafanya kazi ya kuboresha elimu, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya, wanataaluma na wanasayansi wanaoshughulika na ugonjwa wa siko seli. Inashughulika na kufanya tafiti zinazotumika katika tiba ikiwemo upimaji wa ugonjwa wa siko seli kwa watoto wachanga, matumizi ya dawa zakuzuia maambukizi kwa wagonjwa wa siko seli na kuongeza matumizi ya dawa za hydroxyurea. Inafanya hivyo kwa kushirikiana na miradi mingine Afrika na Marekani.
Kwa ujumla, maendeleo chanya kwenye sekta ya afya na tafiti yataletwa na ushirikiano miongoni mwa wanataaluma, watafiti na watunga sera. Ushawishi wa kutosha ni nyenzo muhimu katika kufikia lengo hili
Makala haya yameandaliwa na Prof Julie Makani, mbobezi katika tiba na utafiti wa ungonjwa wa siko seli, akishirikiana na Raphael Z Sangeda, Obiageli Nnodu, Victoria Nembaware, Alex Osei-Akoto, Vivian Paintsil, Emmanuel Balandya, Jill Kent, Lucio Luzzatto, Solomon Ofori-Acquah, Olofunmi I Olopade, Kisali Pallangyo, Irene K Minja, Mario Jonas, Gaston K Mazandu, Nicola Mulder, Kwaku Ohene-Frempong na Ambroise Wonkam.