- Tangazo -
Home Maoni ya MwanaSayansi Korona na tafiti: Umuhimu wa umakini kwa waandishi wa habari Tanzania

Korona na tafiti: Umuhimu wa umakini kwa waandishi wa habari Tanzania

- Tangazo -

Tuanze na maswali 7 ya msingi kuhusu tafiti na uandishi wa habari Tanzania, hasa kwa kuzingatia mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) katika nchi 223 duniani, ikiwemo Tanzania.

  1. Je! Kila utafiti uliofanywa na kuchapishwa katika majarida ya kisayansi, tovuti au mitandao yakijamii unafaa kuandikiwa habari katika chombo chako ili kuifikia jamii?
  2. Je shirika la afya duniani (WHO) liliposema “hakuna ushahidi kwamba waliopona UVIKO-19 hawawezi kuambukizwa tena, Je, shirika hilo lilimaanisha kwamba “waliopona ugonjwa huo hawawezi kamwe kuambukizwa tena?”
  3. Kuna tafiti zilifanywa na watafiti nguli duniani na hapa nchini Tanzania ambazo zingeweza kupotosha jamii? Zilikufikia katika mtindo gani? Ulizitambua? Ulishawishika kuziandikia habari katika chombo chako?
  4. Utafiti ukionyesha kuwa jambo X lina uhusiano na jambo Y, je hilo humaanisha kwamba jambo X husababisha jambo Y?
  5. Je! Unafahamu hatua za msingi ambazo utafiti unapitia ili kukidhi vigezo vyakuwa tafiti za kutumika katika sera za nchi, afua na kuleta mabadiliko au kutunga miongozo ya utoaji huduma?
  6. Je! Kauli ya mwanasayansi au daktari mmoja inatosha kutumika kama msingi wa habari unayoiandaa kuhusu UVIKO-19, ugonjwa mwingine au jambo lolote la kisayansi?
  7. Unapokuwa unaandika habari kuhusu utafiti wa kisayansi, je unategemea habari katika vyombo vya habari vya kimataifa na baadae kutafsiri kwenda katika chombo chako? Huwa unajitahidi kuutafuta utafiti wenyewe na kuwauliza maswali wanasayansi wengine katika fani husika?

Maswali haya yameibuka kutokana na mwenedo wa uandishi wa habari nchini Tanzania na kwingineko, hasa katika kipindi hiki na cha nyuma ambapo Tanzania na karibu dunia nzima imekuwa ikikabiliana na janga la UVIKO-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona. Kwa lugha ya kiingereza unaitwa COVID-19, kama ulivyobatizwa na jopo la wanasayansi kutoka WHO.

Tangu kuibuka kwa ugonjwa huu mwaka juzi (2019) nchini Uchina, wanasayansi mbalimbali duniani wamekuwa wakichakata tafiti, tena kwa kasi kubwa sana.

Hadi kufikia Februari mwaka huu, machapisho zaidi ya 200,000 kuhusu UVIKO-19 yamewekwa katika kanzi data ya shirika la afya duniani. Machapisho haya yanahusu chanzo cha ugonjwa huu, kirusi cha korona, namna kirusi kinavyosambaa, kinavosababisha kifo, namna yakutambua mgonjwa, vipimo, dawa, mbinu za kujikinga, chanjo na uhusiano uliopo kati ya UVIKO-19 na magonjwa mengine.

Unawezaje kuingia kwenye mtego wa upotoshaji?

Kumbuka kuwa UVIKO-19 ni ugonjwa mpya ulimwenguni kote. Uwepo wa tafiti nyingi kuhusu janga la ugonjwa huu umetoa fursa kwa tasnia ya habari kuzalisha habari kwa wingi. Hatahivyo, kuna maswali mengi yanayohitaji majibu ya kisayansi na uchunguzi bado unaendelea kuhusu huu ugonjwa, kupitia tafiti mbalimbali.

Kuchakatwa kwa tafiti mbalimbali kuhusu UVIKO-19, tena kwa kasi kubwa, kwa upande mwingine kumeongeza hatari ya kutolewa kwa taarifa za kisayansi zisizo na ukweli unaojitosheleza au zenye kupotosha. Tafiti zinapofanyika katika hali ya uharaka, kuna hatari ya kukusanya taarifa zisizo na ukweli, kutoa mahitimisho yasiyo thabiti na kuipotosha dunia kwa kutoa mapendekezo yasiyo sahihi.

Kutokana na wanasayansi wengi kukimbilia kuchapisha, kumekuwepo na kufurika kwa tafiti ambazo zimegundulika badae kuwa zilikuwa chini ya viwango. Tafiti hizi zimekuwa zikiwekwa kwenye majarida kama pre-print, yaani chaptisho la mapema linalotangulia mapitio rasmi ya wanasayansi wenza kabla ya kuchapishwa rasmi katika jarida la kisayansi na baada ya kupitiwa kwa kina.

Katika kipindi hiki cha janga la korona, machapisho mengi yameweza kupenya nakutolewa kama habari katika vyombo vya habari, kabla ya mapitio ya mwisho. Hili limeleta mkanganyiko kubwa kwa vyombo vya habari na kwa jamii kwa ujumla. Watafiti wanasema preprint ni nzuri kwa sayansi lakini yaweza kuwa mbaya kwa jamii.

Waandishi wa habari wengi hawakuweza kutambua kwamba tafiti hizi zilikuwa bado zinahitaji kupitia mchakato wa ziada. Hivyo, habari walizowalisha wananchi kupitia vyombo vyao hazikutaja kuwa utafiti husika ulikuwa bado haujahitimishwa kikamilifu. Hatari yake nikwamba utafiti ule ukikosa uthibitisho katika hatua ya miwsho inakuwa vigumu kuiaminisha jamii kitu kingine baada ya kulishwa habari ya mwanzo. Kama mwandishi wa habari ataona kuna ulazima wa kutumia pre-print, inashauriwa kutaja, tena kwa ukubwa, akitoa tahadhari kwamba utafiti huo bado haujafikia mwisho.

Mwaka jana pekee machapisho zaidi ya 1,650 yaliondolewa katika majarida yakisayansi kwasababu mbalimbali ikiwemo kukosa ushahidi thabiti katika mahitimisho. Hali hii inategemewa kuendelea mwaka huu.

Kwa mfano, hitimisho la jarida maarufu duniani la Lancet juu ya dawa ya chloroquine lilipuuzwa badae, baada ya tafiti nyingi zilizofuatia kubaini kuwa dawa hiyo haina tija katika matibabu dhidi ya UVIKO-19. Licha yakuwa ni tiba iliyotiliwa shaka, kituo cha televisheni cha Fox, nchini Marekani kilionekana kuupigia debe utafiti ule.

 

Rais wa Marekani wa wakati huo Donald Trump aliuamini na kuupa kipaumbele katika jamii aliyokuwa anaiongoza. Idadi ya watu waliokuwa wanatumia chloroquine iliongezeka kwa kasi. Kuna madaktari wengi walioamua kutoa dawa hiyo ya chloroquine kwa wagonjwa wao. Baade utafiti ulitupiliwa mbali.  Unaweza kufikiri nini kingetokea iwapo serikali zinngetoa maelekezo kwa madaktari kuanza kutibu wagonjwa wa UVIKO-19 bila kuwa na ushahidi wakutosha kisayansi?

Kwakuwa vyombo vya habari vya Tanzania huwa vinatumia habari kutoka katika vyombo vya habari vya magharibi na kutafsiri habari hizo kwa Kiswahili, kuna hatari yakuingia katika mtego wa kupotosha jamii bila kujua au bila makusudi.

Ushauri: Ni muhimu kwa waandishi wa habari wa Tanzania kufuatilia kwa kina na kuuliza maswali mengi zaidi kwa wanasayansi mbalimbali pale wanapokuwa katika kufanya maamuzi yakihabari juu ya utafiti husika.

Mwandishi anaweza kuuliza maswali yafuatayo:

  • Je! Utafiti huu umefanyiwa mapitio na wanasayansi tofauti tofauti?
  • Umechapishwa katika jarida linaloaminika kisayansi? Kuwa makini na hili pia. Swali linalofuata linaweza kukusaidia.
  • Je! Wasomi wengine wanauamini kwa kiasi gani utafiti huo?
  • Nani amefadhili huo utafiti huo? Kuna wafadhili huwa wanaaminika zaidi katika kufadhili michakato ya tafiti. Wapo ambao hawaaminiki. Uliza wanasayansi au fuatilia kwa undani.
  • Sifa za aliyefanya na kuchapisha utafiti huo ni zipi? Hili litakusaidia kujua kama ni mtaalamu katika eneo hilo au la.
  • Utafiti ni wa mwaka gani? Tafiti za miaka ya zamani zinaweza zisiwe zinahusika na mabadiliko yasasa.
  • Waliofanya na kuuchapisha utafaiti huo wana mgongano wa kimaslahi?
  • Ukubwa wa sampuli ukoje? Mfano, kama idadi ya watu walioshiriki kwenye utafiti ni kubwa, uwezekano wa kuwa sahihi pia ni mkubwa.
  • Mbinu walizotumia kufanya utafiti huo (methodology) zinaeleweka?
  • Matokeo ya utafaiti wao yanaendana na takwimu zilizotolewa?

Habari unayoiandika inauthibitisho wa kisayansi?

Mei 20 mwaka 2020, wafuatiliaji wa habari katika tovuti nchini Tanzania walisoma habari yenye kichwa: Dawa ya corona yathibitishwa Tanzania, inaponya na kansa “Watu hawatokufa tena.” Habari hii iliwekwa kwa msisitizo kabisa kwamba dawa hiyo “yathibitishwa”….na “inaponya”…na “watu hawatokufa tena.” Japokuwa uthibitisho wa dawa kuponya na kuonyesha matokeo ya watu kutofariki ni jambo la kisayansi, habari ile haikuonyesha ushahidi wowote wa kisayansi.

Hadi leo hii, hakuna dawa ambayo imethibitika kikamilifu kwamba inatibu au kuponya UVIKO-19. Tunafahamu kwamba sayansi ni muunganiko wa ujuzi unaozalishwa baada ya miaka mingi ya utafiti na kazi ngumu kutoka kwa wanasayansi mbalimbali. Waandishi wa habari wanaweza kuripoti matokeo mapya ya sayansi au kutumia uelewa wa kisayansi uliopo kuelezea hali mbalimbali za kijamii au mada inayovuma.

Sayansi ndiyo mzizi wa ufanyaji maamuzi. Tungefahamu vipi kama madaktari watoe au wasitoe dawa ya chloroquine kwa wagonjwa wa UVIKO-19? Ni kupitia sayansi tu ambapo wanasayansi wanaweza kuthibitisha kuwa dawa ya zamani au mpya ni salama na ina ufanisi katika kutibu au la.

Hivyo, habari zitakazoandikwa kuhusu korona Tanzania, inashauriwa zizingatie utafiti wa kisayansi. Kwa mfano, waandishi wanapoandika kuhusu utaratibu au amri yakujifungia ndani (lockdown), wanazingatia utafiti au muktadha? Tafiti zinasemaje kuhusu “lockdown” kwenye nchi za Afrika? Ni wakati gani amri hiyo itekelezwe au isitekelezwe? Lingine ni kuhusu uvaaji wa barakoa. Je, watu wavae barakoa na glavu? Je ni aina gani za barakoa zitumike, wakati gani, kwa muda gani n.k?

Maswali haya na maswali mengine ambayo yanaumiza vichwa vya watunga sera, wataalmu na watu binafsi yanaweza kujibiwa kupitia tafiti za kisayansi. Kwa upande mwingine, waandishi wa habari wakipuuzia sayansi, inaweza kuwa gharama kwa jamii. Ni kweli kwamba jamii hupenda kusoma habari zinazohusu watu, lakini kukiwa kuna hatimisho lolote linalohitaji uthibitsho kisayansi, ni muhimu kuzingatia maoni yakitaalamu kutoka kwa manasayansi kwa kuzingatia utafiti katika eneo hilo.

X husabaisha Y. Uthibitisho uko wapi?

Je, uhusiano au uwiano ni sawa na sababu? Nitoe tu mfano wakubuni. Umekutana kichwa cha habari. “Unywaji wa gongo husababisha maambukizi ya magonjwa ya zinaa.”

Pia ukakutana na kingine: “Unywaji wa gongo unahusishwa na hatari kubwa ya maambukizi ya zinaa.”

Msomaji mwenye busara anaweza kutambua kuwa kichwa cha habari cha kwanza kilimaanisha cha pili: kwamba kunywa gongo nyingi kunaweza (kwa njia ya kuongeza uwezekano wa kujamiiana) kunaongeza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa.

Waandishi wa habari wanatakiwa kutoa habari kwa usahihi. Bila kuwa makini na kutambua utofauti wa mambo haya muhimu katika mahitimisho yanayotolewa kisayansi, wanaweza kuipotosha jamii.

Kwa mfano. Mwezi Machi mwaka 2020, mitandao ilifurika taarifa kuwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB), yaani BCG inaweza kuwalinda watu dhidi ya UVIKO-19. Hii nadharia ilitokana na machapisho matatu yaliyoonyesha kuwa maambukizi ya virusi vya korona yalikuwa kwa kiasi cha chini katika baadhi ya nchi zinazotumia chanjo ya BCG. Kutoa hitimisho kuwa BCG ni sababu ya kiasi kidogo cha maambukizi ya virusi vya korona kwa baadhi ya nchi, siyo sahihi. Ni sawa nakusema kunywa gongo husababisha maamukizi ya magonjwa ya zinaa. Kwenye hilo swala la BCG, shirika la afya duniani lilitoa ufafanuzi kuwa hakuna ushahidi kuwa chanjo ya BCG inawalinda watu dhidi ya UVIKO-19. Hatahivyo, ripoti ya WHO ilionyesha kwamba kulikuwa na dosari katika utafiti huo iliyohusisha chanjo ya BCG na uwepo wa kasi ndogo ya maambukizi ya virusi vya korona. Tafiti zilichapishwa mtandaoni bila kupitiwa kwa kina na jopo la wanasayansi (yaani preprint).

Je, kuna wanasayansi waasi?

Katika sayansi, maafikiano yanahitajika baina ya wanasayansi ili kuthibitisha ukweli. Haya makubaliano ya pamoja ndiyo hujenga msingi  wa sayansi. Lakini kuna baadhi ya wanasayansi ambao huenda kinyume na taratibu za kufikiana kuhusu makubaliano ya jumla kisayansi. Wanasayansi huasi taratibu zilizowekwa katika kuwasilisha mawazo yao na huamua kuwasilisha kupitia mitandao ya kijamii, tovuti na vyombo vingine maarufu vya habari. Kwa mfano, kuna wanasayansi ambao taarifa zao zinaenda kinyume kabisa na makubaliano ya jumla miongoni mwa wanasayansi kuhusu chanjo dhidi ya UVIKO-19. Hii husababisha baadhi ya watu kwenye jamii kuwaamini waasi hao na kuacha kutumia chanjo. Jambo hili lina madhara makubwa katika afya ya jamii. Magonjwa kama surua ambayo huzuiwa kwa chanjo yanaweza kulipuka tena.

Soma: Chanjo dhidi ya korona: Fahamu mchakato wa uvumbuzi, majaribio na matumizi

Kwa kipindi hiki cha janga la UVIKO-19, habari zenye mlengo tofauti zimejitokeza kwa kiasi kikubwa. Kuna baadhi ya wanasayansi wanatoa hoja kwamba UVIKO-19 sio ugonjwa mkali kulinganisha na mafua ya msimu.Wanasayansi wa aina hii wana haki ya kutoa mawazo lakini nyingi huwa hawana ushahidi wenye nguvu kuthibitisha hoja zao. Kwa waandishi, habari za hawa wanasayansi waasi zinaweza kuonekana zina nguvu na zinavutia kihabari.  Hapa ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa makini na wanasayansi wa namna hii na kuhoji kwa undani utafiti wao ili kubaini kama kweli una ushahidi wakutosha.

Kama hakuna ushahidi maana yake nini?

Ukiumwa na ukaenda hospitali, daktari anaweza kuhisi umeugua malaria lakini hawezi kuwa na uhakika hadi pale atakapopata ushahidi kwamba damu yako ina vimelea vinavyosababisha malaria. Atakuandikia kipimo uende maabara kupimwa damu. Mtaalamu wa maabara asipokuta vimelea hivyo katika damu, ripoti yake kwa daktari itasema hakukuta vimelea katika sampuli yako ya damu. Basi. Hatasema hauna malaria kwasababu kuna uwezekano kukawa na kiasi kidogo cha vimelea lakini kipimo hakikuweza kuvitambua. Hiyo ndiyo sayansi. Na ndivyo ushahidi wa kisayansi unazungumzwa. Wataalamu wa WHO waliposema kuwa bado hakuna ushahidi kwamba wagonjwa wa UVIKO-19 wanaopona hawawezi kuambukizwa tena virusi vya korona, hawakumaanisha kuwa watu hao kamwe hawawezi kuambukizwa tena. Ila tu nikwamba hapakuwa na ushahidi wowote kuthibitisha hilo kwa wakati huo.

Hivyo, inabidi kuzingatia kwamba kuwapo kwa machapisho mengi kuhusu UVIKO-19 kunatoa fursa kwa waandishi wa habari kuandika kuhusu sayansi ya ugonjwa huu. Ingawa kulingana na kasi ambayo tafiti zinafanyika, waandishi wanashauriwa kuwa makini na tafiti wanazokutano nazo.

- Tangazo -
Syriacus Buguzi
Syriacus Buguzi
Syriacus Buguzi is a Science Journalist who is passionate about raising the profile of Tanzania’s scientific research output and innovation through mass media. He is a medical doctor (MD) but currently pursuing a Masters in Science Communication at the University of Sheffield in the United Kingdom.
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -