Dunia bado inaendelea kushuhudia madhara ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya korona (UVIKO-19). Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani, watu takribani milioni 104 wameambukizwa na milioni 2.3 wamepoteza maisha tangu ugonjwa ulipotangazwa China mwaka mmoja uliopita.
Mojawapo ya njia zinazoweza kutumika kudhibiti maambukizi ya huu ugonjwa ni pamoja na kuepuka sehemu zenye msongamano wa watu, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni na matumizi ya barakoa.
Pia katika siku za karibuni, kuna chanjo zimegunduliwa na kujaribiwa katika mataifa mbalimbali yaliyoendelea na kuthibitishwa kisayansi kuwa ni salama na zina uwezo wa kuulinda mwili wako dhidi ya virusi vya korona kwa asilimia 75 hadi 95 kwa wale waliokamilisha utaratibu wa chanjo kama ulivyopangwa.
Mpaka sasa, mataifa mbalimbali katika nchi zilizoendelea yameanza kutoa chanjo ya kujikinga na UVIKO-19 kwa raia wake ambao wako katika hatari zaidi.
Watu wengi wanauliza, lakini mbona chanjo zimeharakishwa?
Pamoja na jitihada zinazoendelea, uvumbuzi wa chanjo hizi umefanyika kwa kasi kubwa na kuleta wasiwasi kuhusu usalama wake. Kumbuka kwamba dunia iko katika dharura. Wengine wameenda mbali na kusema kwamba labda ni mpango wa kuwadhuru watu, hasa katika nchi zinazoendelea au ni mpango wa biashara ya kuuza chanjo.
Tetesi hizi zimefanya baadhi ya mataifa yanayoendelea, kusita kufanya mipango ya kujihusisha na chanjo hizi. Hizi tetesi pamoja na kuleta taharuki, hazina uthibitisho pamoja na ukweli ulio wazi kuwa hizi chanjo zimefanyiwa utafiti kwa kufuata miongozo ya mamlaka za udhibiti za nchi husika na shirika la afya duniani. Ikumbukwe kuwa ugonjwa bado upo na unazidi kuleta changamoto ulimwenguni kote.
Katika mijadala mbalimbali inayofanyika kwenye mitandao ya kijamii, ni dhahiri kuwa kuna ombwe kubwa la uelewa kuhusu mchakato wa ugunduzi, utafiti na usambazaji wa chanjo.
Chanjo ni mojawapo ya njia bora na rahisi za kuzuia magonjwa. Shirika la afya duniani linakadiria kwamba vifo takribani milioni 3 vinazuiwa kila mwaka kwa matumizi ya chanjo zinazotumika kuzuia magonjwa kama surua, pepopunda, kifua kikuu, dondakoo, kuharisha, nimonia nk.
Chanjo hupitia hatua zipi hadi kufaa kwa matumizi ya binadamu?
Kuna michakato mbalimbali inayopitiwa ili kuhakikisha hizi chanjo siyo kuwa tu zina uwezo wa kumkinga binadamu dhidi ya magonjwa, bali pia zinakuwa salama kwa mtumiaji.
Kabla tafiti za chanjo hazijafanyika, ni sharti watafiti kupeleka mpango wao wa utafiti kwa mamlaka za udhibiti ili kuupitia na kuangalia mantiki za kisayansi zilizomo. Mpango hukikidhi vigezo nawatafiti hupewa kibali cha kuanza utafiti.
Tafiti za awali kabisa huwa ni kuangalia usalama wa chanjo, na uwezo wake wa kuchochea kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa uliolengwa. Hatua hii huwa inafanyika kwa wanyama kama panya au ngedere ili kujua ni kwa jinsi gani hawa wanyama wanaweza kustahimili hiyo chanjo. Hatua hii inapoisha na matokeo kuchakatwa, huwa yanapelekwa kwenye mamlaka za udhibiti kwa ajili ya kuyapitia na kujiridhisha.
Je, ikitokea utafiti ukawa haukidhi vigezo?
Iwapo itagundulika kuwa haina madhara makubwa na ina uwezo wa kuchochea kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa unaofanyiwa utafiti, mamlaka hutoa kibali cha kuendelea na hatua ya pili. Isipokidhi viwango (usalama na uwezo wa kuchochea kinga ya mwili) utafiti unasimamishwa.
Iwapo utafiti utafanikiwa kuingia hatua inayofuata (hatua ya kwanza kwa binadamu), watu wachache (chini ya 100) huwa wanashiriki kupewa chanjo. Watu hawa hujitolea. Hatua hii ni kwa ajili ya kuangalia usalama na uwezo wa chanjo kuchochea kinga kwa binadamu. Katika kipindi chote cha utafiti, taarifa za washiriki waliopata chanjo huwa zinafuatiliwa na baadhi ya vipimo huwa vinachukuliwa kuhakikisha hakuna madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.
Wakitambua madhara wanachukua hatua gani?
Tatizo lolote analopata aliyepata chanjo huwa linafuatiliwa ili kujua kama limesababishwa na chanjo au kitu kingine. Iwapo itadhibitika kuwa zaidi ya asilimia 10 wamepata madhara makubwa kwa sababu ya chanjo, sharti utafiti usimame na uchunguzi mpya ufanyike au utafiti kusimamishwa moja kwa moja.
Huwa kuna bodi za usalama wa chanjo zinazopitia hizi takwimu mara kwa mara wakati utafiti unaendelea. Kama awamu itamalizika salama, takwimu huchakatwa na matokeo yake huwa yanapelekwa kwa mamlaka ya udhibiti kwa ajili ya mapitio na kuangalia kama inafaa kuingia awamu inayofuata. Kama matokeo yatakuwa yanaridhisha, kibali kinatolewa kuendelea na hatua ya pili kwa binadamu.
Kuchochea kinga ya mwili
Hatua ya pili huwa ni kwaajili ya kuangalia zaidi usalama, uwezo wa kuchochea kinga ya mwili, na dozi ya chanjo. Katika awamu hii, washiriki huongezeka kwa sababu usalama wake unakuwa umeanza kuthibitika lakini hatua zote za kiusalama zinafanyika kama ilivyokuwa hatua ya kwanza, na matokeo yakiwa tayari yanapelekwa kwa mamlaka za udhibiti kwa ajili ya kupitiwa, yakikidhi, kibali cha kuingia awamu ya tatu huwa kinatolewa.
Hatua ya tatu huwa inahusisha watu wengi zaidi (maelfu) na huwa unafanyika sehemu nyingi tofauti ili kujua usalama wa chanjo na uwezo wa kuchochea kinga ya mwili kwa watu kutoka makundi tofauti na mazingira tofauti. Mara nyingi hatua hii huwa inachukua muda mrefu zaidi kutegemea na kasi ya maambukizi ya ugonjwa uliolengwa.
Katika hatua hizi, huwa kuna juhudi kadhaa zinafanyika ili kuweza kugundua madhara ya chanjo mapema, na ikiwezekana kusimamisha utafiti. Hatua hizi ni pamoja na kuchanja watu wachache, na kukaa muda kabla ya kuchanja watu wengine, mapitio ya mara kwa mara na bodi za usalama wa chanjo, kufuatilia kwa karibu wagonjwa wanaopata chanjo na kutambua madhara yanayojitokeza baada ya chanjo na kupeleka ripoti ya usalama wa chanjo na takwimu kwa mamlaka ya udhibiti mara kwa mara katika kipindi chote cha utafiti.
Iwapo itagundulika kwamba kuna walakini katika usalama, utafiti huwa unasimamishwa. Ila iwapo madhara huwa ni machache na madogo ambayo huwa yanaisha baada ya muda mfupi kama maumivu au kuvimba sehemu ya chanjo, mwili kuchoka au homa, uchambuzi wa faida na hasara ya kutumia au kutotumia chanjo huwa unafanyika, na iwapo faida itakuwa kubwa kuliko madhara, chanjo huwa inaendelea kutumika.
Majaribio ya chanjo huwa yanakwama katika hatua gani?
Ni chini ya asilimia 3 tu ya majaribo ya chanjo yanayofanikiwa kupita hatua ya tatu. Nyingi huwa zinaishia njiani kwa kutokuwa salama au kushindwa kuthibitisha uwezo wa kuzuia maambukizi.
Pale utafiti unapoisha, matokeo huwa yanachakatwa, yanachapishwa kwenye majarida na pia kupelekwa tena kwenye mamlaka ya udhibiti kwa ajili ya mapitio. Iwapo yatakidhi vigezo vilivyowekwa, watafiti huendelea na utaratibu wa kusajili chanjo na kuanza kuisambaza kwa wale wahitaji (hatua ya nne).
Nchi mbali mbali zinaweza kujiridhisha kuhusu usalama?
Huwa ni jukumu la kila nchi kupitia mamlaka ya udhibiti kupitia hizo chanjo na kujiridhisha usalama wake. Kwa nchi ambazo hazina uwezo huo, shirika la afya duniani huwa linasaidia kuzihakiki. Hata baada ya chanjo kuidhinishwa, huwa ni jukumu la kampuni iliyotengeneza dawa kwa kushirikiana na mamlaka za udhibiti, mpango wa taifa wa chanjo na watoa huduma ya chanjo kuhakikisha wanakusanya taarifa zote zinazohusiana na madhara ya chanjo na kutoa taarifa za usalama wa chanjo mara kwa mara (mara nyingi huwa ni kila baada ya miaka mitano ).
Ikitokea nchi ikagundua walakini?
Chanjo inaweza kufungiwa muda wowote na mamlaka za udhibiti iwapo taarifa za kiusalama zitagundulika.
Hivyo basi, ni dhahiri kuwa uvumbuzi, utafiti na usambazaji wa chanjo huwa ni mchakato ambao usalama wa chanjo unapewa kipaumbele katika hatua zote. Pia mamlaka na bodi mbali mbali huwa zinahusika kuhakikisha usalama wa watu wanaoshiriki katika tafiti zinalindwa.
Hatuna budi kuunga mkono juhudi zinazofanyika katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza kupitia chanjo, kushiriki katika ugunduzi na utafiti wa chanjo, kuepuka kueneza taarifa zisizo sahihi kuhusu chanjo na kuwezesha mamlaka za udhibiti kuhakiki chanjo na kufuatilia mara kwa mara taarifa za usalama wa chanjo ambazo tayari zimeidhinishwa na zinatumika nchini.
[…] Chanjo dhidi ya korona: Fahamu mchakato wa uvumbuzi, majaribio na matumizi […]
Ndiyo, chanjo ambazo tayari zimeanza kutumika, zina uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia kupata dalili kali za ugonjwa kwa asilimia zaidi ya 90.Ambacho bado kinafanyiwa utafiti ni kinga inakaa muda gani.
[…] Chanjo dhidi ya korona: Fahamu mchakato wa uvumbuzi, majaribio na matumizi […]