Je, wewe ni miongoni mwa watu wanaoogopa sindano hususani wakati wa kuchomwa chanjo? Huenda unatafuta kujua ni namna gani utaweza kukabiliana na hisia unazopata juu ya maumivu ya sindano wakati wa kupata chanjo au pre pain kwa lugha ya Kiingereza.
Fahamu kwamba hauko peke yako. Robert Mallya ni Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Kati ya watu 10 anaowachoma sindano katika taasisi hiyo, wawili kati yao huonyesha hofu kuhusu kuchomwa sindano.
Hata baadhi ya wahudumu wa afya huonyesha woga wakati wakuchomwa sindano, anasema Mallya. “Inawezekana wakawa na hofu ile ya kuonekana kabisa, mwingine anajikaza lakini wengine wanapiga kelele hata kabla ya kuchomwa.”
Mallya anarejea takwimu kutoka JKCI zinazoonyesha kuwa kati ya watu 1000 waliokwenda kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika taasisi hiyo, ni watu watano pekee waliogopa sindano.
Kwingineko, hofu ya kuumia kwa sindano inaweza kuelezea takriban 10% ya visa vya watu kusita kuchomwa chanjo ya UVIKO-19. Kukabiliana na hofu hiyo kunaweza kuongeza ufanisi katika mipango ya chanjo, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Cembridge nchini Uingereza umebaini.
Huenda wewe ni miongoni mwa wale wanaosita na pengine hivi sasa unatafuta taarifa ambazo zitakusaidia kujua jinsi ya kuepuka hisia za maumivu au hofu juu ya sindano ya chanjo. Ili uweze kufanya maamuzi sahihi, wataalamu wanabainisha yafuatayo:
Pata taarifa sahihi kuhusu chanjo
Kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo na umuhimu wake kwa afya ya jamii ni miongoni mwa mambo ambayo wanasayansi wanasema yatakusaidia kuepuka hisia za hofu wakati na baada ya kuchoma sindano ya chanjo.
Pelagia Batorolimi ni Afisa Muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es-Salaam, mwenye uzoefu wa miaka 15 akitoa huduma hiyo hospitalini hapo.
Anasema ipo haja na zipo faida mtu huzipata pale anapoamua kwenda hospitalini kuonana na wataalamu, kupatiwa elimu sahihi na uelewa kuhusu chanjo mbalimbali.
“Sindano tunayotumia [katika chanjo ya UVIKO-19] ni ile ile tunayotumia kama ilivyo kwa chanjo nyingine, kutakuwa na maudhi madogo madogo labda mkono kuhisi mzito na kuuma kidogo,” anasema Batorolimi.
Ni muhimu kumuomba mtaalamu akupe elimu sahihi kabla yakukuchoma chanjo. Wale wanaouliza, hupewa maelekezo muafaka. “[Tunaelekeza] pia namna gani anaweza kufanya, kukabiliana na maumivu na huwa yanaisha kabisa,” anasema Batorolimi.
Chuja taarifa, hasa za mitandaoni
Wataalamu wa afya wanasema kuwa taarifa zinazotia woga zinaweza kukujengea hisia za maumivu na hofu juu ya sindano za chanjo.
“Lazima tuwe na uwezo wa kuchuja zile taarifa zinazopatikana kwenye mitandao, zipi ni sahihi, zipi zimeongezwa chumvi. Ukishindwa kuzichuja njoo kwetu sisi wataalamu tutazungumza na wewe tutakusaidia kupata uhalisia,” anasema Mallya.
Anatoa mfano aliouona kwenye mitandao yakijamii wenye picha jongefu zikionyesha mtu anachoma sindano inayoonekana kuwa na bomba kubwa sana na mtu anapiga kelele.
[Hii] imepelekea watu kuogopa lakini kiukweli ni sindano ndogo, haina maumivu lakini ikitokea umehisi maumivu, tunashauri kunywa [dawa yakupunguza maumivu]…”
“Tuwe watu wa kutafuta taarifa maeneo sahihi [na] hata kama ni mitandao ya kijamii tuangalie ile ambayo [inaaminika].
“Ikiitokea umepata taarifa kwenye mitandao au sehemu nyingine yoyote na huna uhakika nayo, fuatilia kwa ukaribu na hata kwa wataalamu unaowafahamu, ndipo uchukue hatua na tusipende kusambaza taarifa ambazo hatuna uhakika nazo (si sahihi,),” anashauri.
Pia, kuzungumza na watu wengine hasa wale wa karibu yako, waliochoma sindano ya chanjo ni mbinu nyingine unavyoweza kuitumia, kwani itakusaidia pia kupata uzoefu wao na hata kukusaidia kuondokana na hisia unazokabiliana nazo.
Japo utafiti zaidi unahitajika ili kufahamu ni watu wangapi wanaogopa sindano na wanaogopa nini hasa, uzoefu unaonyesha kuwa wapo watu huogopa sindano yenyewe.
“Ukitoa ile sindano (kwenye kihifadhi chake) mtu anaiona kwenye macho yake anaiangalia ni ndefu, unakuta anaanza kuhisi hofu kwamba hiki kitu kinaingia kwenye mwili wangu, unakuta ‘automatically’ mtu anaogopa,” anaeleza Mallya.
Jiandae kisaikolojia
Dkt Frank Msafiri ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Anasisitiza kuwa ni muhimu kufanya maandalizi binafsi ya kujijenga kisaikolojia pale unapotaka kufanya maamuzi ya kwenda kupata chanjo.
“Maumivu ni madogo sana, yaani hasa pale sindano inapoingia, kwa hiyo inakuwa sana ni kwa mtu binafsi kujiandaa,” anasema Dkt. Msafiri.
Anaongeza “Hii (hisia za maumivu) inatofautiana kati ya mtu na mtu na si watu wengi ambao hukabiliana na hali hiyo, ndiyo maana ni muhimu mtu binafsi kujiandaa kisaikolojia.”
Usikaze mkono
Ukishaishinda hofu juu ya maumivu ya sindano, jambo jingine linalohimizwa kuepuka wakati wa kuchomwa sindano hiyo ni kukaza misuli (ya mkono/ mwili).
Mallya anasema kuwa, wapo watu ambao hujawa na hisia za woga nakuanza kutetemeka pale wanapojua tu kwamba mchomaji wa sindano anakaribia kuanza.
“Lakini si kwamba ameshawahi kupata ile ‘experience’ ya maumivu… hamna ni uwoga tu. Mtu wa namna hii [huwa] tunamhakikishia ili kumuondolea hofu asiogope yale maumivu ya ile sindano,” anabainisha.
Anasema si rahisi pia kuhisi maumivu makali kwenye eneo la bega kama vile mtu anapochoma sindano kwenye ncha ya kidole, ikiwa mtaalamu anayekuchoma sindano atabinya vizuri sehemu ya msuli unaopeleka taarifa kwenye ubongo ili kuupa mwili mrejesho wa kuhisi maumivu.
“Kuna kitu kinaitwa ‘nerve endings’ (kule mwisho wa mishipa ya fahamu), kule huwa kuna maumivu makali kuliko sehemu zingine ndiyo maana ninasema ukija kwa mtaalamu anajua jinsi ya kukushika na kukubinya vizuri.
“Ile ‘nerve’ unakuwa umeibinya kidogo isipeleke maumivu makali kwenye ubongo, unakotafsiriwa ili kupelekea kwenye taarifa ya maumivu,” anabainisha.
Anasema wataalamu huzingatia pia kumuandaa mtu kisaikolojia pale wanapotaka kumchoma sindano na hiyo humsaidia mwili wake kujiandaa na kuondokana na hisia za hofu na maumivu.
“… Inamsaidia ‘ku-relax’, kutokuwa na ile hali ya kuogopa inayompeleka kujikaza sana na kukaza misuli,” anasema.
Anaongeza “Akikaza maana yake (mchomaji) utatumia nguvu kuichoma, lakini ‘aki-relax’ utakuta inaingia vizuri sana, hatasikia maumivu makali sana na wakati mwingine atauliza kama tayari umeshachoma, unamwambia ndiyo anashangaa.
Angalia pembeni
“Wakati wa kuchomwa [mtu] anaweza kuangalia pembeni na si kuitazama ile sindano, kama mtu unavyoenda kung’oa jino kuna sindano ya ganzi, kama ganzi inapoingia unahisi maumivu kidogo baada ya hapo unatoka bila [kuhisi] maumivu,” anasema Dkt Msafiri.