- Tangazo -
Home Afya Mbu wanapojificha wakati wa upuliziaji dawa ndani ya nyumba:utafiti

Mbu wanapojificha wakati wa upuliziaji dawa ndani ya nyumba:utafiti

- Tangazo -

Dar es Salaam. Mbu wanaosambaza vimelea vya ugonjwa wa malaria hupendelea kujificha na kupumzika katika maeneo yasiyofikiwa na dawa ya kuua wadudu wakati wa upuliziaji ndani ya nyumba, utafiti umebaini.

Zaidi ya asilimia 93 ya Watanzania wanaishi katika maeneo ambayo ni hatarishi kwa maambukizi ya vimelea vinavyosababisha malaria,  kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani(WHO).

Dawa za kuua wadudu mara nyingi hutumika katika bara la Afrika, hususani nchini Tanzania kwaajili ya kuua mbu wanaopumzika katika kuta ndani ya nyumba na wakati mwingine kwenye paa na dari.

Lakini, kupitia utafiti uliochunguza tabia za jamii mbili kuu za mbu jike wasambazao malaria (Anopheles funestus na Anopheles arabiensis), watafiti kutoka Tanzania wamebaini kuwa mbu hao pia hupendelea kupumzika kwenye sakafu, samani (fenicha), nguo zilizotundikwa na hata vyombo vya chakula. Maeneo haya, mara nyingi hayalengwi wakati wa upuliziaji dawa za kuua wadudu, watafiti wanasema.

Kwa miaka mingi, watafiti wanasema, mbinu za upuliziaji dawa za kuua wadudu ndani ya nyumba hazikuboreshwa, pamoja kuwepo kwa ukuaji wa teknolojia, hususani katika ujenzi wa nyumba za kisasa; ikizingatiwa pia kuwa mbu wanazidi kubadili tabia zao.

Utafiti huu umeonyesha kuwa asilimia 40 hadi 60 ya mbu 17,870 waliofanyiwa uchunguzi, hupumzika katika maeneo ambayo kwa kawaida hayapewi umuhimu wakati wa upuliziaji dawa ndani ya nyumba; huku uwiano mkubwa ukiwa katika nyumba zilizoezekwa kwa bati.

Utafiti unapendekeza ufanyike uboreshwaji wa upuliziaji dawa za kuua wadudu katika nyumba zilizoezekwa kwa bati, na kuongeza: “…Taratibu za sasa za upuliziaji dawa za kuua wadudu zilifanyika miongo kadhaa iliyopita wakati nyumba nyingi barani Afrika zikiwa bado zimeezekwa kwa nyasi.”

Mtafiti kiongozi wa utafiti huo, Betwel Msugupakulya, kutoka Idara ya Afya ya Mazingira na Sayansi ya Ikolojia, Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) nchini Tanzania, anasema matokeo ya utafiti huo yanapasa kuwahimiza watoa maamuzi katika sekta ya afya kuhakikisha mbinu bora za upuliziaji madhubuti wa dawa za kuua wadudu ndani ya nyumba.

“Ni imani yetu kwamba ufahamu uliopatikana katika utafiti huu utatoa mwanga katika mipango ya kukuza umadhubuti wa kupambana na mbu waenezao malaria nchini Tanzania  na barani Afrika,” anasema Msugupakulya.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sayansi wa IHI, Dkt Fedros Okumu, ambaye ni mtafiti mwenza, matokeo ya utafiti huo hayana maana kwamba kama dawa za kuua wadudu zinapulizwa kwenye kuta za nyumba, kemikali zilizomo kwenye dawa hizo hazitaleta madhara kwa mbu wapunzikao mbali na kuta hizo.

“Hii, hata hivyo, ni ishara kwamba tabia za mbu wasambazao vimelea vya malaria kupumzika ndani ya nyumba inaonekana ni changamoto katika kutokomeza malaria; kama vile ilivyo upuliziaji dawa za kuua mbu ndani ya nyumba,’’ Dkt Okumu alisema.

“Tunasisitiza uboreshaji wa upuliziaji dawa za kuua mbu ndani ya nyumba ufanyike, ambao utapunguza usambazaji wa mimelea vya malaria,” aliongeza kusema.

Utafiti huo, uliochapishwa katika Jarida la Malaria (Malaria Journal) January15, 2020, ulifanywa kwa takriban miezi kumi na moja katika vijiji vinne vya wilaya za Ulanga na Kilombero mkoani Morogoro, kusini mashariki mwa Tanzania.

Wakati wa utafiti, watafiti hao waliwatumia wataalamu kukusanya  mbu kutoka kila nyumba wakitumia vifaa maalum vinavyoweza kukusanya wadudu (Prokopack aspirators).

Mbu hao walikusanywa kutoka kila kijiji nyakati za mchana na jioni kwa siku tano za kila juma (wiki).  Kwa kuepuka kuingilia faragha za watu nyakati za jioni na usiku wa manane mbu walikusanywa na wanakaya waliopewa mafunzo maalumu.

Paa za nyumba zilizoezekwa na nyasi na makuti au bati na zenye kuta za udongo au matofali au kupigwa plasta za zege ndizo zilizolegwa zaidi.

Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Taifa ya utafiti katika Tiba(Nimr), Dkt Deus Ishengoma anasema utafiti huu ni muhimu katika jitihada za kutokomeza malaria, ingawa anasisitiza kuwa elimu kwa umma inahitajika kwenye upuliziaji dawa za kuuwa wadudu.

“Wananchi waelimishwe namna ya kutambua maeneo ambayo mbu hupenda kupumzika ndani ya nyumba. Pia, kuwepo na uhamasishaji katika ujenzi wa majengo yasiyoweza kuruhusu mbu kuingia na kupumzika ndani ya nyumba,’’ anashauri Dkt Ishengoma.

- Tangazo -
MwanaSayansi
MwanaSayansihttps://sayansi.medicopress.mediai
MwanaSayansi ni chanzo mahususi cha habari, maoni na uchambuzi kuhusu sayansi na teknolojia nchini Tanzania; hasa katika nyanja ya maendeleo. Taarifa zote na maudhui huzingatia sera na taratibu za MedicoPRESS, asasi iliyoanzishwa kwa lengo la kukuza ujuzi wa waandishi wa habari na wanasayansi katika kuwasilisha taarifa za kitabibu na kisayansi kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -
  1. Hayo Maeneo ambayo ayapuliziwi dawa yanatakiwa yapuliziwe lakini njia sahihi za kudhibiti madhara kwa binadamu Zitafutwe kabla ya upuliziaji,kujenga nyumba bora iwe ni mojawapo ya njia njia za kuzuia malaria, jitihada iwe kubwa Sana katika kuharibu mazalia ya mbu na pia mazalia ya mbu yasiwepo ,mwisho usimamihaji wa sheria za utunzaji bora wa mazingira uzingatiwe nyakati zote. Tafiti yenu ni nzuri Sana kwa umma wa Tanzania na afrika

  2. Nafikiria huu Ni ujumbe mzurj kwa watu wanaohusika na maswala ya mazingira lKn za Kuna mratibu was malaria anae simamia ,swala kupulza dawa za kuuwa mbu:kwa wilaya ,lkn pia maafisa afya kuendelea kutumia hi.ripoti ya utafiti kuelimisha jamii!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -