- Tangazo -
Home Afya Matumizi holela ya ‘antibaotiki’ kwa watoto wenye kuhara yadhibitiwe: watafiti

Matumizi holela ya ‘antibaotiki’ kwa watoto wenye kuhara yadhibitiwe: watafiti

- Tangazo -

Dar es Salaam. Matumizi holela ya dawa za viuavijasumu (antibaotiki) kwa watoto wenye kuhara husababisha madhara zaidi kwa watoto hao, wataalamu nchini Tanzania wamesisitiza, huku wakishauri hatua madhubuti zichukuliwe ili kudhibiti matumizi ya dawa hizo.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), wanasisitiza kuwa watoto wanaougua magonjwa ya kuhara wanapaswa kutibiwa kwa Zinki, dawa ya maji ya kunywa yenye chunvi (ORS), na kupata chakula stahiki, badala ya kuwatibu kwa dawa hizo za viuavijasumu.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani(WHO), kuna matukio karibu bilioni 1.7 ya ugonjwa wa kuhara utotoni kila mwaka duniani. WHO pia inasisitiza kuwa ugonjwa wa kuhara unazuilika kwa kunywa maji safi na salama na kuzingatia usafi wa vyoo.

Mtaalamu mwandamizi wa magonjwa ya watoto kutoka Muhas, Dkt Rodrick Kisenge, anasema dawa kama metronidazole, erythromycin, azithromycin, niloxamide na ciprofloxacin zinazidi kutumika kimakosa miongoni mwa jamii na watoa huduma, katika kutibu watoto wenye kuhara

Akiwasilisha mada katika kongamano lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Muhas na Chuo kikuu cha Havard, Dkt Kisenge alisema,“Mashambulizi makali ya kuharisha maji maji(acute waterly diarrhoea) kwa watoto yanasababishwa zaidi na maambukizi ya virusi au na vimelea vingine ambavyo havihitaji kutibiwa kwa dawa za viuavijasumu [antibaotiki],’’ alisema Dkt Kisenge.

Kongamano hilo lililenga kuonyesha ukubwa wa tatizo la magonjwa ya kuhara miongoni mwa watoto nchini Tanzania na jinsi ya kusonga mbele katika kuyadhibiti.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu(Nimr), Professa Yunus Mgaya, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kidhibiti magonjwa ya kuhara hasa kwa watoto hususani kwa kuhimiza chanjo ya Rotarix.

Hadi kufikia mwaka 2015, Tanzania ilikuwa imepunguza vifo vitokanavyo na kuhara miongoni mwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, kwa asilimia 89 kutoka vifo 35.3 miongoni mwa vizazi hai 1000 mwaka 1980, hadi vifo 3.9 miongoni mwa vizazi hai 1000 mwaka 2015. Hizi ni takwimu za Benki ya Dunia.

“Licha ya hatua zote hizi, bado tunahitaji kuweka mkazo zaidi kuyatokomeza,’’ alisema.

Katika kongamano hilo, Dkt Kisenge alitoa matokeo ya awali ya majaribio ya utafiti uliolenga kuonyesha kama dawa ya antibaotiki (Azithromycin) inaweza kupuguza vifo na kuboresha ukuaji miongoni mwa watoto wanao hara damu na wanaoishi katika maeneo yasiyokuwa na huduma za afya za kujitosheleza. Matokeo kamili ya utafiti huo uliofanywa nchini Tanzania yanategemewa kuchapishwa hivi karibuni, alisema.

Hata hivyo, alionyesha kutokukubaliana na majaribio ya ufafiti wa mwaka 2018 uliohusisha watoto karibu 200,000 katika nchi za Malawi, Tanzania na Niger, ambao ulihimiza usambazaji na matumizi kwa kiasi kikubwa ya dawa za antibaotiki(Azithromycin) kwa watoto.

Utafiti huo, ulisema kwamba dawa za antibaotiki zinapaswa kutolewa kwa watoto kwa kiwango kikubwa kama mkakati wa kupunguza vifo miongoni mwa watoto wachanga.

Kwa mujibu wa Dr Kisenge, utafiti huo uliochapishwa katika jarida la New England Journal of Medicine ungechochea usugu wa vimelea vya bakteria kwa dawa hiyo na huo usugu ungekuwa ni tatizo kubwa katika mfumo wa afya endapo matokeo yake yangeingizwa katika sera na matumizi.

Taarifa zinaonesha kuwa baadae WHO ilitilia shaka utafiti huo, lakini iliziruhusu nchi saba ikiwemo Tanzania kufanya majaribio ambayo matokeo yake ya awali hayapendekezi matumizi ya dawa za antibaotiki, Azithromycin, kwa kiasi kikubwa katika watoto, kama ilivyo kwenye utafiti wa 2018.

Alitumia wasaa huo katika kongamano kushauri jamii na watoa huduma za afya kuzingatia matibabu sahihi kwa watoto wenye kuhara, huku akirejea tafiti mbalimbali zinazoonyesha kuwa asilimia 44 ya watoto wasioharisha damu katika nchi zenye kipato cha chini wanaripotiwa kupewa dawa za antibaotiki kama sehemu ya matibabu ya ugonjwa huo.

“Dawa za antibaotiki hupendekezwa kwa watoto waliogundulika kuhara damu, hata hivyo, tafiti zinaonesha kwamba hili halizingatiwi,’’ anasema Dkt Kisenge.

“Hali pekee ambayo watoto wanaoharisha wanaweza kutibiwa na dawa za anitibaotiki ni pale mtoto anapokuwa na utapiamlo uliokithiri, kipindupindu, ugonjwa wa kuhara damu au wakati mtoto huyo huyo amegundulika kuugua homa ya mapafu (pneumonia),” alisema.

Akizungumza wakati wa warsha hiyo, mtaalamu mwandamizi wa magonjwa ya watoto kutoka Muhas, Professa Karim Manji, aliwahimiza wafanyakazi wa afya nchini kote kuepuka utoaji ambao si sawa wa dawa za antibaotiki ili kuiokoa Tanzania na dunia kwa ujumla kutokana na janga la kutofanyakazi kwa dawa hizo.

“Ni muhimu kwamba wafanyakazi wa afya wapatiwe taarifa muhimu zinazohusiana na matumizi ya dawa hizi.  Hii itakuwa hatua kubwa katika kuokoa maisha, kuweka sawa matumizi ya dawa za kuua sumu mwilini na kupunguza hatari ya dawa kutofanyakazi,” alisema Proffesa Manji.

- Tangazo -
MwanaSayansi
MwanaSayansihttps://sayansi.medicopress.mediai
MwanaSayansi ni chanzo mahususi cha habari, maoni na uchambuzi kuhusu sayansi na teknolojia nchini Tanzania; hasa katika nyanja ya maendeleo. Taarifa zote na maudhui huzingatia sera na taratibu za MedicoPRESS, asasi iliyoanzishwa kwa lengo la kukuza ujuzi wa waandishi wa habari na wanasayansi katika kuwasilisha taarifa za kitabibu na kisayansi kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -