- Tangazo -
Home Afya Je, umepona ugonjwa wa korona lakini dalili haziishi?

Je, umepona ugonjwa wa korona lakini dalili haziishi?

- Tangazo -

Huenda wewe ni mmoja kati ya hawa. Ulipata maambukizi ya virusi vya korona na kuugua kwa wiki kadhaa. Ulipata changamoto katika kupumua, homa ikawa juu na kadharika. Kwa bahati nzuri, watoa huduma za afya wakakupigania na ukapata matibabu stahiki, hivyo baada ya muda ukaanza kupata ahueni. Baada ya kadhia yote hiyo, ukaambiwa na daktari wako kuwa hauna tena virusi hivyo ndani ya mwili wako. Furaha ikatawala. Lakini baada ya muda, ukaanza kustajabu.

Na unajiuliza: “Mbona bado nahisi kichwa kugonga, misuli inauma, mwili umenyong’onyea na siwezi kutuliza fikra zangu juu ya jambo moja na wakati mwingine naweza kusahau mambo na akili yangu ni kama imezingirwa na ukungu?”

Je sayansi inasemaje kuhusu hili?

Unachokipitia ni hali inayoanza kuonekana kwa baadhi ya wagonjwa wa waliopona Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), pale ambapo dalili za ugonjwa huo huzidi kujitokeza licha ya kuwa mtu ametibiwa na amepona.

 

Wakati watu wengi waliopata maambukizi ya korona hupata dalili kwa muda mfupi na kupona, kuna baadhi ya watu hubaki wanasumbuliwa na dalili za muda mrefu. Tatizo hili linatambulika kama korona ya muda mrefu au mabaki ya muda mrefu ya dalili za ugonjwa a korona. Kitaalamu tatizo hili linaitwa Post-Acute Sequelae of SARS-CoV-2 infection au Post-Acute Sequelae of COVID-19 (PASC).

Je, mabaki ya dalili baada ya maambukizi ya korona ni nini?

Hizi ni dalili ambazo baadhi ya watu huendelea kuishi nazo baada ya kupona maambukizi ya korona. Kwa kawaida watu wenye dalili za wastani za ugonjwa huu hupona ndani ya wiki 1 hadi 2 baada ya kupata maambukizi lakini watu wenye tatizo hili hubaki na baadhi ya dalili kuzidi wiki 12 tangu wapate maambukizi.

Tafiti kuhusu tatizo hili bado zinaendelea lakini tafiti kutoka nchini Uingereza zimeonyesha kuwa watu 3  kati ya 10 walioruhusiwa kutoka hospitali baaada ya kupona UVIKO-19 walibaki na dalili mbalimbali za muda mrefu. Tafiti za nchini marekani zimeonyesha tatizo hili lipo kwa asilimia 20 hadi 80.

Soma zaidi: Korona na tafiti: Umuhimu wa umakini kwa waandishi wa habari Tanzania

Je dalili hizi za muda mrefu baada ya kupona korona ni zipi?

Kutokana na tafiti za ufuatiliaji wa wagonjwa waliopona UVIKO-19, imeonekana kuwa dalili zinazobaki kuwasumbua watu wengi ni pamoja na uchovu, kukosa pumzi baada ya shughuli ndogo au kutembea kidogo, mabaki ya kikohozi kisichoisha, maumivu ya misuli, maumivu kwenye maungio, maumivu ya kifua, kuhisi akili ina ukungu unaomfanya mtu kushidwa kufikiri vizuri na kutuliza fikra katika mambo fulani, sonona na hali ya huzuni, maumivu ya kichwa, moyo kwenda mbio na pamoja na changamoto za kupata usingizi.

Kwa nini baadhi ya watu hubaki na dalili za muda mrefu baada ya kupona ugonjwa wa korona?

Mpaka sasa haifahamiki kwa asilimia 100 kwa nini baadhi ya watu hupona kabisa dalili zote za UVIKO-19 ndani ya muda mfupi na wengine hubaki wakitaabika na dalili za muda mrefu. Nadharia mojawapo ni kwamba dalili za muda mrefu hutokana na majeraha ya kudumu kwenye viungo vya mwili kama mapafu na moyo kutokana na virusi vya korona. Nadharia hii inaweza kuthibitishwa kwa uwepo wa makovu kwenye mapafu ya baadhi ya wagonjwa waliopona ugonjwa wa korona.

Pia dalili hizi zinaweza kutokana na ugonjwa wa uchovu wa mwili unaosababishwa na maambukizi ya virusi ambao hutambulika kama Myalgic Enephalomyelitis. Vilevile baadhi ya watu hupata sonona au hali ya huzuni kutokana na tatizo la msongo utokanao na mtu kuugua ugonjwa mkubwa ikiwemo kulazwa au kuwekwa kwenye mashine ya kusaidia kupumua, hali hii huleta msongo mkali kwa baadhi ya wagonjwa.

Je ufanye nini unapopatwa na dalili za muda mrefu baada ya kupona ugonjwa wa korona?

Ni jambo la muhimu sana kubaki ukiwa na mawasiliano ya karibu na mtoa huduma wako wa afya na kuzingatia ushauri wote aliokupatia wakati wa ruhusa. Unapoona dalili mbaya kama kushindwa kupumua ni muhimu kuwahi kurudi kituo cha kutolea huduma za afya kwa uangalizi wa karibu na uchunguzi.

Soma zaidi: Njia za kuimarisha kinga yako dhidi ya maambukizi

Lakini unaweza boresha afya yako ukiwa nyumbani ikiwemo kuzingatia lishe bora hasa kula matunda na mboga za majani, kujitahidi kupata usingizi wa kutosha, kufanya mazoezi kulingana na uwezo wako na ushauri wa daktari kulingana na hali yako, kutotumia vileo kama sigara au pombe.

Ni muhimu watu kuelewa kuwa elimu hii inalenga la kuongeza uelewa wa watu kuhusu UVIKO-19, lakini hailengi kukufanya upuuze ushauri na maelekezo uliyopewa na mtoa wako wa afya. Zingatia maelekezo ya mtaalamu wako wa afya.

Rejea:https://clinicaltrials.gov/ct2/show/record/NCT04362150?view=record

- Tangazo -
Dkt Norman Jonas
Dkt Norman Jonashttp://www.sayansi.africa
Medical Doctor | Internal Medicine - Kilimanjaro Christian Medical University College | Health Communication
- Tangazo -

Tufuate

570FansLike
330FollowersFollow
100SubscribersSubscribe

Makala Mpya

- Tangazo -

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Tangazo -