Unaweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) endapo utatambua tofauti kati ya taarifa potofu na sahihi, wanasayansi wanasema.
Kukithiri kwa taarifa potofu kuhusu chanjo ya UVIKO-19, hususani katika mitandao yakijamii kumeibua maswali mengi na sintofahamu miongoni mwa jamii, huku wanasayansi wakitahadharisha kuhusu athari za taarifa potofu.
Ukweli ni upi kuhusu kuganda kwa damu?
Taarifa zilisambaa duniani kote baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa baadhi ya watu wachache waliopata chanjo ya AstraZeneca walidai kupata athari za kuganda kwa damu, yaani kutokea kwa mabonge ya damu yasiyo ya kawaida kwenye ubongo.
Chanjo hiyo imeendelea kutolewa katika nchi mbalimbali baada ya wanasayansi kubaini kuwa hakuna uthibitisho kuwa kuganda kwa damu kulitokana moja kwa moja na chanjo hiyo.
Hatahivyo, UVIKO-19 au magonjwa mengine yanaweza kusababisha kuganda kwa damu, anasema Dkt Elisha Osati, daktari bingwa katika tiba ya magonjwa ya ndani-kitengo cha mapafu na moyo, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Dkt Osati anasema taarifa za kisayansi zilizopo hadi sasa zinaonyesha kwa watu waliosema walipata athari yakuganda kwa damu walifanyiwa uchunguzi na ikagundulika baadhi walikuwa na matatizo mengine kiafya.
Anasema, ukilinganisha na matatizo mengine ya afya, uwezekano wakutokea athari yakuganda kwa damu kutokana na chanjo ni asilimia ndogo sana na hizo athari ni nadra. “Inakadiriwa kuwa asilimia 0.004,” anasema Dkt Osati.
Chanjo inaweza kubadili mfumo wako wa vinasaba (DNA)?
“Suala la chanjo kubadilisha genetiki[ya binadamu] halina ukweli wowote,’’ anasema Dkt Daniel Maeda, Mhadhiri katika Idara ya Biolojia na Bioteknolojia ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi-Chuo Kikuu cha Dar es-Salaam.
Maswali mengi kwenye jamii kuhusu chanjo na vinasaba (DNA) yamejikita hasa kwenye chanjo aina ya Pfizer na Moderna, ambazo hutumia teknolojia ya mRNA.
Kwa mijibu wa Dkt Maeda, hakuna muingiliano kati ya mRNA na vinasaba (DNA) vya watu wanaopewa chanjo hizo.
Sayansi inaonyesha kuwa teknolojia ya mRNA hutumia alama za chembechembe za jeni ya urithi kutoka kwenye virusi. Alama hizi hufundisha seli za mwili wako kujenga kinga dhidi ya virusi vya Korona na hivyo kuusaidia mwili kudhibiti UVIKO-19.
Pia, chanjo ya Janssen, kutoka kampuni ya Johnson & Johnson, iliyoanza kutumika nchini Tanzania hutumia virusi (modified adenovirus) ambavyo vimebadilishwa ili visiweze kukufanya uwe mgonjwa, haviwezi kujizidisha ndani ya mwili wako, haviwezi kuingia kwenye DNA yako na haviwezi kukufanya uugue.
Kiini cha kirusi hicho hutuma ishara kuamsha seli za kinga zilizo karibu kwenye mwili wako na hivyo kufanya seli ya mwili wako kutoa protini ili kujenga kinga dhidi ya UVIKO-19.
“Huu ni mfumo wa siku nyingi. Hakuna kitu kipya,” anaeleza Dk Maeda.
Ukiwa umechanjwa unaweza kuambukizwa?
Ndiyo. Mtu anapochanjwa dhidi ya UVIKO-19 bado anaweza kuambukizwa tena virusi hivyo, kwani lengo la chanjo hadi sasa siyo kuzuia maambukizi, bali kumkinga binadamu dhidi ya madhara ya ugonjwa.
Dkt Osati anasena, “chanjo inasaidia mtu kutokupata ugonjwa mkali ambao ungeweza kumsababishia madhara makubwa au hata kifo.”
Mtaalamu huyo wa mafapu anatahadharisha kwa kutoka mfano kuwa, “Mapafu yakiharibika nivigumu kurudi katika hali yake ya kawaida,” huku akiitaka jamii kuchangamkia chanjo ya UVIKO-19.
“Pia kuchukua tahadhari ni muhimu sana. Licha yakuchanjwa, ni lazima kuvaa barakoa,kunawa mikono kwa maji tiririka na kuepuka misongamano kwasababu bado maambukizi yapo na yanaweza kuenea zaidi,’’ anaonya.
Wenye magonjwa ya kudumu hawahitaji chanjo?
Uvumi umesambaa katika mitandao yakijamii kwamba watu wenye magonjwa yakudumu, hususani kisukari au maradhi ya moyo, hawapaswi kupata chanjo, ikidaiwa kuwa wakichanjwa watadhurika.
“Huo ni uvumi tu,” anasema Dkt Mariam Amour, Mhadhiri katika Afya ya Jamii, kutoka Chuo Kikuu kishiriki cha Afya na Sayansi Muhimbili (MUHAS).
“Watu hawa[wenye magonjwa yakudumu] ndio hasa wanatakiwa kupata chanjo kwani kinga zao za mwili zinakuwa zimeshuka. Mfano, watu wenye kisukari wanashauriwa kupata chanjo kwasababu kinga yao ya mwili iko nchini, kwahiyo chanjo inasaidia kuongeza kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mengine,’’ anasema Dkt Amour.
“Nawashauri jamii waendelee kujifunza na wawasikilize wataalamu, kuwaelewa na kukubali kupata chanjo,”anasema.
Hii ni chanjo ya majaribio?
Kuibuka kwa chanjo dhidi ya UVIKO-19 kumesifiwa sana kama njia yakuweza kutokomeza janga, hatahivyo, mchakato wakuetengeneza chanjo hizo umeibua wasiwasi kwa baadhi ya watu katika jamii, huku wengine wakidhani bado iko katika majaribio.
Chanjo zinazotumika hivisasa dhidi ya UVIKO-19 haziko katika hatua ya majaribio, anasema Dkt Julieth Sebastian, Mkufunzi kutoka Taasisi ya Afya ya Jamii-Chuo Kikuu kishiriki cha Kilimanjaro (KCMUCo).
Anasema tangu siku nyingi kumekuwepo na kirusi cha Korona (SARS CoV-1) ambacho kimekuwa kikifanyiwa utafiti.
“Hivyo, tafiti nyingi za kuelewa kirusi zilikwishakufanywa hata kabla ya UVIKO-19 kutokea. [Janga hili lilipoanza,] tafiti ziliboreshwa kwaajili yakupata chanjo hizi tulizonazo.”
Kawaida, mchakato wakutengeneza chanjo huwa ni mrefu na wa gharama kubwa kwa sababu ya ucheleweshaji unaosababishwa na kuomba ufadhili, idhini ya maadili, kuajiri watakaojitolea, kujadiliana na wazalishaji na kuongeza uzalishaji.
Lakini pia, katika hali ya dharura ya janga la UVIKO-19 wanasayansi, madaktari, bodi za idhini ya maadili, wazalishaji na wakala wa udhibiti wote wamekuja pamoja ili kufanya kazi kwa bidii na haraka.
Mhariri: Dkt Syriacus Buguzi kwa kufuata sera ya uhariri ya MedicoPRESS.